Mashabiki Man United waishangaa familia ya Glazers

Muktasari:
- Familia ya Glazers ilinunua hisa za Man United miaka 20 iliyopita kutoka kwa wawekezaji wa Jamhuri ya Ireland, JP McManus na John Magnier.
MANCHESTER, ENGLAND: MASHABIKI wa Manchester United wamesikitishwa sana baada ya kugundua familia ya Glazer imewekeza kiasi kidogo sana cha pesa tangu walipoanza kuimiliki timu hiyo hadi sasa.
Familia ya Glazers ilinunua hisa za Man United miaka 20 iliyopita kutoka kwa wawekezaji wa Jamhuri ya Ireland, JP McManus na John Magnier.
Wakati wanachukua hisa kutoka kwa matajiri hao tayari walikuwa wamiliki wa asilimia 30 ya klabu, lakini baada ya hapo ziliongezeka hadi kufikia asilimia 57.
Baada ya kuchukua hisa kutoka kwa Magnier na McManus, walinunua pia hisa za tajiri wa Scottland, Harry Dobson na wakafikisha hisa za asilimia 62.
Waliendelea hivyo na ilipofikia Juni 2005 walifanikiwa kuwa wamiliki rasmi wa timu hiyo baada ya kuwa na hisa za asilimia 98.
Hata hivyo, hadi kufikia sasa tangu mwaka 2013, mashabiki wengi wamekuwa hawafurahishwi na kile ambacho kinatokea kwa timu hiyo huku wengine wakidai hakuna uwekezaji wa maana unaofanywa.
Huenda malalamiko yao juu ya uwekezaji yakawa ya kweli kwani ripoti kutoka tovuti ya Athletic, familia ya Glazers ambayo imeichukua timu hii kwa Pauni 800 milioni kwa muda wote huo wa miaka 20, imetoa Pauni 45 milioni pekee kutoka kwenye mifuko yao.
Kiasi hicho kinaonekana kuwa ni kidogo ikilinganishwa na timu nyingine, mfano Ipswich Town iliyopanda daraja msimu huu, mmiliki wao amewekeza Pauni 83 milioni, Southampton wamewekeza Pauni 85 milioni huku Bournemouth pia wakiwekeza Pauni 93 milioni kutoka kwenye mifuko ya wamiliki wao.
Kijumla wawekezaji wa Chelsea ndio wamewekeza pesa nyingi zaidi kutoka kwenye mifuko yao ambapo baada ya kuinunua timu hiyo mwaka 2022 kwa Pauni 2.5 bilioni, waliwekeza Pauni 146 milioni ndani ya misimu miwili ikiwa ni karibia mara tatu ya kile ambacho Glazers wamewekeza kwenye miaka 20.
Matajiri wa Manchester City wao tangu wainunue timu hiyo mwaka 2008 wawekeza Pauni 1.3 bilioni na timu inayokaribia ni Fulham ambayo wamiliki chini ya Shahid Khan wamewekeza Pauni 788 milioni.
Inaelezwa pesa nyingi zinazotumiwa Man United zimekuwa zikikopwa na familia hii hali inayosababisha timu ibakie na madeni makubwa yanayotokana na riba.
Hata hivyo, licha ya ukosefu wa uwekezaji, Manchester United wameonekana kuwa na matumaini mapya baada ya kuingia kwa Sir Jim Ratcliffe ambaye amenunua hisa za asilimia 25 na ndio amepewa majukumu ya kusimamia shughuli zote za mpira wa miguu kwenye timu hiyo.