Martin Keown afichua usajili Arsenal

Muktasari:
- Mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo na kapteni wao Pierre-Emerick Aubameyang hadi sasa ndio straika pekee aliyefikisha mabao zaidi ya 20 tangu msimu wa 2019/20.
LONDON, ENGLAND: LEJENDI wa Arsenal, Martin Keown, amefichua kwamba timu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa London tayari imesaini mkataba na mshambuliaji mpya ili kuboresha eneo lao la ushambuliaji.
Mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo na kapteni wao Pierre-Emerick Aubameyang hadi sasa ndio straika pekee aliyefikisha mabao zaidi ya 20 tangu msimu wa 2019/20.
Alexander Isak kutoka Newcastle ni miongoni mwa wachezaji wanaohusishwa na Arsenal, huku pia kukiwa na uvumi kuhusu Viktor Gyokeres na Dusan Vlahovic.
Alipohojiwa kuhusu hitaji la Arsenal la mshambuliaji mpya, Keown alisema kuwa usajili wa Isak unaweza kuwa mgumu, lakini usajili wa mchezaji mwingine kwa fedha nyingi huenda ukafanyika.
Akizungumza na TNT Sports, Keown alisema: “Napatwa na hisia kuwa kwa sasa Isak itakuwa ngumu kumpata hususani baada ya Newcastle kushinda lile kombe (Carabao),”
“Dunia nzima inajua kuhusu hilo. Kuna mkurugenzi mpya wa michezo sasa, atatakiwa aangalie wachezaji na kusajili mastaa wapya wazuri ikiwezekana kwa bei ya chini, asiwezekeze katika kutumia fedha nyingi.”
Keown ana imani kubwa kuwa Arsenal itasaini mshambuliaji katika miezi ijayo, na amedai kuwa usajili huo tayari umefanywa.
“Ningependa kusema kuwa mchezaji tayari amenunuliwa na jambo hilo tayari limemalizika. Hawawezi kufanya makosa tena.”
Hata hivyo, Keown anaamini kuwa ukosefu wa mchezaji anayehakikisha mabao umekuwa kiini cha matatizo ya Arsenal msimu huu, lakini Jamie Carragher, mchezaji wa zamani wa Liverpool, hakubaliani na hilo. Carragher anadhani kuwa matatizo ya Arsenal ni ukosefu wa ubunifu kwani hawatengenezi nafasi za kutosha.