Manchester City bado mambo magumu

Muktasari:
- Hata hivyo, mechi hiyo haikumuacha kocha wa Man City, Pep Guardiola bila maumivu tu, lakini imemuacha akiwa na majeraha kadhaa kichwani na puani yaliyotokana na kujikwangua kwa kucha bila kutarajia.
MANCHESTER, ENGLAND: MAMBO bado ni magumu kwa kikosi cha Manchester City, baada ya kukubali sare ya mabao 3-3 katika mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Feyenoord ya Uholanzi, jana usiku.
Hata hivyo, mechi hiyo haikumuacha kocha wa Man City, Pep Guardiola bila maumivu tu, lakini imemuacha akiwa na majeraha kadhaa kichwani na puani yaliyotokana na kujikwangua kwa kucha bila kutarajia.
Kinachoonekana, kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya kisaikolojia ni kwamba, matokeo mabovu ambayo timu hiyo imeendelea kuyapata katika mechi za karibuni yamegeuka kuwa msalaba kwa kocha huyo mwenye mbinu na mikakati mingi ya ushindi.
Man City inakabiliwa na kundi kubwa la wachezaji ambao ni majeruhi, huku ikidaiwa kwamba nyota wake waliopo wengi wao wanacheza wakiwa na majeraha sambamba na uchovu unaotokana na kucheza mechi mfululizo.
Dhidi ya Feyenoord jana, Pep alikubali kubebeshwa lawama akidai anastahili baada ya kuongoza kwa mabao 3-0 hadi dakika ya 53, kabla ya kibao kugeuka kuanzia dakika ya 75 na kumlazimisha kushikilia bomba ili asipoteze mechi yake ya sita ya mashindano msimu huu.
Man City ilimaliza kipindi cha kwanza ikiongoza kwa mabao ya Erling Haaland aliyefunga kwa penalti katika dakika ya 44, kisha akatupia jingine ile ya 53 kufuatia bao la dakika ya 50 la Ilkay Gundogan.
Hata hivyo kibao kilianza kugeuka kuanzia dakika ya 75 kwa bao la winga Mualgeria Anis Hadj Moussa aliyefunga kwa shuti la mbali kabla ya Santiago Gimenez kutupia dakika ya 82 na David Hancko kusawazisha ile ya 89.
Kama kawaida, licha ya mabao hayo ya wageni yaliyotokana na mashambulizi, Man City ilicheza mpira wake wa kumiliki wote wa mchezo ikiongoza hadi mwisho kwa asilimia 64 dhidi ya 36 za wageni.
Hata hivyo, wakati wote wa mchezo Pep alionekana amechoka na mara moja moja akitoa maelekezo kwa wachezaji wake tofauti na alizoweleka.
Baada ya mchezo kocha huyo alisema anabeba lawama kwa timu yake kupata sare ilhali ilikuwa katika nafasi nzuri ya kuondoka na ushindi, huku akifichua jinsi alivyoumia pua akiwa pia na alama nyekundu kichwani.
Pep ambaye kabla ya mchezo alisema anawakosa nyota wake sita wa kikosi cha kwanza, alionyesha kukerwa na kiwango cha wachezaji waliocheza.
Alipoulizwa kuhusu jeraha kwenye pua na alama nyekundu kichwani wakati wa mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi, kocha huyo alisema: “Ndiyo! Ni kutokana na (kujikwangua na) kucha yangu ya kidole. Nilijikwangua kwa kucha yangu.
Kocha huyo alilalamikia kushindwa kwa timu yake kupata ushindi baada ya Feyenoord kufunga mabao matatu katika dakika 14 za kipindi cha pili na kumshangaza.
“Hatuwezi kushinda michezo,” alikiri Guardiola. “Kama timu, kila mara tumekuwa tukipata njia za kushinda kwa miaka mingi. Hivi sasa hali ni tofauti, hakuna kinachotokea.”
City ambao walivunja mfululizo wa mechi tano bila ushindi watashuka kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya vinara wa Ligi Kuu England, Liverpool utakaopigwa katika Uwanja wa Anfield bila ushindi kwa zaidi ya mwezi mmoja.
“Haikuwa lazima kusema chochote kwao - wanajua vizuri sana,” alisema Guardiola, alipoulizwa aliwaambia nini kwa wachezaji wake.
“(Feyenoord) hawakuturuhusu kushinda. Hali iko hivyo na ni vigumu sana kukubali. Utakuwa msimu mgumu kwetu na tunapaswa kukubali. Tunapaswa kuwapa morari wachezaji. Mimi napaswa kufanya hivyo. Ni kazi yangu.”
Guardiola alifanya mabadiliko matatu dakika ya 69 wakati City wakioongoza kwa mabao matatu akiwapumzisha Kevin De Bruyne, James McAtee na Jahmai Simpson-Pusey akiamini kwamba mchezo ulikuwa umemalizika.
“Nathan (Ake) alitoka nje zikiwa zimesalia dakika 20 na sikuwa na hisia zozote kwamba mambo yangebadilika. Nathan amekuwa akiumia mara nyingi. Hatukutaka kumuweka uwanjani kwa dakika 90,” alisema Guardiola.
“Nilifanya hivyo (pia) kwa ajili ya Kevin (De Bruyne) na Macca (McAtee) pamoja na Jahmai (Simpson-Pusey) ili wawe imara zaidi (kwa ajili ya mechi zijazo). Wakati ule ilikuwa vyema kabisa.”
Alipoulizwa kuhusu kuzomewa mwishoni mwa mchezo na baadhi ya mashabiki wa City, Pep alisisitiza kwamba anaelewa ni kwa nini.
“Wamevunjika mioyo. Bila shaka tunaelewa hilo. Wanakuja hapa (uwanjani) siyo kwa ajili ya kukumbuka mafanikio ya zamani, bali kuona timu ikishinda,” alisema.
Sare hiyo imeiacha City ikiwa nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa ikiwa na pointi nane kutokana na mechi tano, huku mechi dhidi ya Juventus, PSG na Club Brugge zikiwa zimebaki.
City pia imeruhusu mabao mawili au zaidi kwenye mechi sita mfululizo kwa mara ya kwanza tangu Mei 1963.
Kocha wa Feyenoord, Brian Priske aliwasifu wachezaji wake kwa ari ya kupambana, lakini akasisitiza kuwa City bado ni timu bora duniani.
“Ilikuwa mechi ya ajabu na jioni ya kipekee dhidi ya timu ambayo kwangu bado ni bora zaidi duniani,” alisema Priske.
“Ni dhahiri wanakumbana na changamoto fulani kwa sasa, ingawa walikuwa wakiongoza 3-0. Walifanya makosa matatu muhimu ambayo tuliyatumia mwishoni. Zilikuwa juhudi za kipekee na ari kutoka kwa wachezaji wetu," alisema.
UTILITY
1989 - DHIDI ya Feyenoord, Manchester City wameshindwa kushinda mechi ambayo walikuwa wanaongoza kwa mabao matatu kwa mara ya kwanza kwenye mashindano yote tangu Mei 1989 dhidi ya Bournemouth wakiwa Ligi Daraja la Pili Englanda (3-3).