Man United yapigwa nyumbani

MANCHESTER, ENGLAND. BAADA ya kuwa na matokeo mazuri katika mechi saba mfululizo za michuano tofauti, ikiwamo ya Ligi Kuu England, timu ya Manchester United jana ilikumbana na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Fulham ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Old Trafford.
Man United inayopambana kuingia kwenye Nne Bora ya ligi hiyo, iliruhusu bao lililowatibulia rekodi katika dakika za nyongeza baada ya mabeki wa timu hiyo kufanya uzembe kumruhusu Alex Iwobi kufunga bao la ushindi, ikiwa ni dakika chache tangu Harry Maguire alipowasawazishia Mashetani Wekundu dakika ya 88.
Wageni walitangulia kwa bao la dakika ya 65 lililofungwa na Calvin Bassey na kuwafanya Man United kupambana kusaka bao la kusawazisha kabla ya Maguire kufunga bao na baadaye dakika ya 90+7 kufanya kosa lililoibeba Fulham.
Matokeo hayo yameibakisha Man United katika nafasi ya sita kwa pointi 44 baada ya mechi 26, wakati Fulham nayo ikiendelea kusalia nafasi ya 12 ikifikisha pointi 32.
Mapema kwenye mechi za ligi hiyo, wenyeji Aston Villa waliifumua Nottingham Forest kwa mabao 4-2, huku Brighton nayo ikikabwa koo nyumbani na Everton kwa kutoka sare ya 1-1, huku Crystal Palace ikaizamisha Burnley iliyokuwa pungufu baada ya Josh Brownhill kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 35, kwa kuifunga mabao 3-0.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja utakaopigwa kuanzia saa 10:30 jioni wakati Wolverhampton itakapoikaribisha Sheffield United katika Uwanja wa Molineux kusaka alama tatu katika michuano hiyo.