Utajiri alioacha Diogo Jota ni huu

Muktasari:
- Tayari ameshazikwa lakini vitu vingi vimeendelea kubakia nyuma yake. Kati ya vile vilivyobakia ni utajiri wake.
PORTO, URENO: WIKI iliyopita dunia ya wapenda soka ilisikitishwa sana na taarifa za kifo cha mchezaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Ureno, Diogo Jota ambaye alifariki dunia katika ajali huko Zamora, Hispania.
Tayari ameshazikwa lakini vitu vingi vimeendelea kubakia nyuma yake. Kati ya vile vilivyobakia ni utajiri wake.
Licha ya kwamba hakuwa katika orodha ya wachezaji 10 wanaolipwa pesa nyingi England, bado fundi huyu ameacha mkwanja wa kutosha. Hapa tumekuletea jinsi alivyokuwa anapiga pesa na mali alizoacha.

AMEPIGAJE PESA
Hadi anafariki dunia ripoti zinadai alikuwa na utajiri unaokadiriwa kufikia dola 30 milioni. Chanzo chake kikuu cha mapato kilikuwa ni mshahara wake aliokuwa anakunja Liverpool.
Wakati anasajiliwa kwa mara ya kwanza alikuwa akilipwa pauni 90,000 kwa wiki lakini ilipofika mwaka 2022, alisaini mkataba mpya ambao ulimwezesha kukunja pauni 150,000 kwa wiki.
Hata hivyo, mshahara huo kwa mwaka wa pauni 8 milioni uliongezeka na kufikia pauni 9 milioni kutokana na bonasi alizokuwa akipata.
Mbali ya pesa alizokuwa anapata kama mshahara na bonasi, pia alikuwa akijiingizia kipato kupitia mikataba ya udhamini na kampuni mbalimbali.
Kwanza ni mkataba wake na Nike ambao walikuwa wakimpa karibia dola 2 milioni kwa mwaka, vilevile alikuwa na mkataba wa ubalozi na kampuni ya EA-Sports.

NDINGA ZAKE
Alimiki magari makali kama Porsche 911 Turbo S - dola 210,000)
Range Rover Sport - dola 120,000)
Lamborghini Huracan - Dola 250,000

MIJENGO
Alikuwa akimili mjengo wa kifahari huko Lisbon ambao unakadiriwa kuwa na thamani ya dola 3 milioni. Ndani ya nyumba hiyo ripoti zinaeleza kulikuwa na chumba maalumu cha kufanyia mazoezi, kiwanja kidogo cha mpira.
Pia katika Jiji la Liverpool alikuwa akiishi katika mjengo wenye thamani ya dola 1.5 milioni ambao alipanga.

MSAADA KWA JAMII
Aliwahi kushiriki mashindano ya ePremier League Invitational mwaka 2020, akishirikiana na wachezaji wengine wa Ligi Kuu England ambapo lengo ilikuwa ni kukusanya mapato na kuyapeleka kwenye shirika la afya la England kusaidia huduma wakati wa janga la COVID-19.
Jota alikuwa akishiriki kwa karibu katika mradi wa Standard Chartered - Futuremakers, ambao ulianzishwa na Liverpool kwa lengo la kusaidia vijana masikini kupitia michezo. Alipewa tuzo maalum kutokana na mchango wake katika mradi huo.
Staa huyu pia aliwahi kusaidia taasisi ya Newham Charity kwa karibu.

MAISHA BINAFSI NA BATA
Alikuwa kwenye ndoa na mwanamama Rute Cardoso aliyemwoa Juni, 22, 2025 ambaye kwa pamoja walibahatika kupata watoto watatu.
Hakuwa anapenda sana kuweka maisha yake katika vyombo vya habari na watu waliokuwa wanaishi karibuni na nyumba yake huko Porto wanaeleza kuwa alikuwa mtu wa kujishughulisha katika shughuli za hisani, pia alishiriki sana katika michezo na sherehe za watoto.