Man United yamtoa Onana kwa Waturuki
Muktasari:
- Makubaliano hayo hayana kipengele cha kumruhusu Trabzonspor kumnunua moja kwa moja baada ya mkopo kumalizika. Hata hivyo, klabu hiyo italipa mshahara wote wa Onana kwa kipindi chote cha mkopo.
LONDON, ENGLAND: KIPA wa Manchester United, Andre Onana amerejea kwa mkopo katika klabu ya Trabzonspor ya Uturuki kwa msimu wa 2026/27.
Makubaliano hayo hayana kipengele cha kumruhusu Trabzonspor kumnunua moja kwa moja baada ya mkopo kumalizika. Hata hivyo, klabu hiyo italipa mshahara wote wa Onana kwa kipindi chote cha mkopo.
Mbali na kugharamia mshahara wake, Trabzonspor pia itailipa Manchester United ada ya mkopo, huku makubaliano hayo yakijumuisha bonasi mbalimbali zinazoweza kupatikana kulingana na mafanikio yatakayofikiwa.
Katika taarifa yake, Manchester United ilisema uhamisho huo unasubiri kukamilishwa kwa taratibu za kibali cha kimataifa na usajili rasmi.
Onana alicheza mechi 29 akiwa Trabzonspor msimu uliopita baada ya kutolewa kwa mkopo na United kufuatia kipigo cha kushtua katika Kombe la EFL dhidi ya Grimsby Town ya League Two mwezi Agosti mwaka jana.
Mchezo huo, ambao United ilipoteza kwa mikwaju ya penalti katika uwanja wa Blundell Park, ulikuwa ndiyo mechi pekee aliyocheza Onana akiwa Manchester United msimu huo.
Alihitimisha msimu kwa mafanikio makubwa baada ya kuisaidia Trabzonspor kutwaa Kombe la Uturuki kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2020.
Onana, ambaye alinunuliwa kutoka Inter Milan mwaka 2023 kwa ada ya pauni47.2 milioni, bado ana miaka miwili iliyobaki katika mkataba wake na Manchester United. Awali alitarajiwa kurejea kambini kwa maandalizi ya msimu mpya tarehe 9 Julai.
Hata hivyo, alifahamu kuwa hakuwa na nafasi ya kumng’oa Senne Lammens, ambaye ni chaguo la kwanza la kocha mkuu Michael Carrick.
Kwa kuwa Lammens yupo na kikosi cha Ubelgiji katika Kombe la Dunia, mustakabali wa kipa namba mbili wa Manchester United, Altay Bayindir, nao bado haujawa wazi.
Wakati huohuo, kipa kijana mwenye matumaini makubwa Radek Vitek anatarajia kupata uhamisho kabla ya maandalizi ya msimu kuanza. Hali hiyo inaweza kumlazimu Carrick kuanza maandalizi akiwa na makipa wasio na uzoefu mkubwa pamoja na mkongwe Tom Heaton, kuelekea mchezo wa kirafiki dhidi ya Wrexham utakaochezwa mjini Helsinki tarehe 17 Julai.