Man United inapiga ndefu kwenda mbele

Muktasari:
- Lakini, kocha wa Manchester United, Ruben Amorim ameamua kuja vinginevyo - akimtaka kipa wake kupiga pasi ndefu.
MANCHESTER, ENGLAND: KWENYE soka la mtindo wa kisasa, timu zote bora zinacheza kwa kupanga mashambulizi yake kuanzia nyuma.
Lakini, kocha wa Manchester United, Ruben Amorim ameamua kuja vinginevyo - akimtaka kipa wake kupiga pasi ndefu.
Na kipa Andre Onana alisajiliwa kutoka Inter Milan mwaka 2023 kutokana na uwezo wake wa kuanzia mpira nyuma.
Lakini, bado amekuwa akifanya makosa makubwa ambayo yamekuwa yakiigharimu timu hiyo.
Hata hivyo, kwa uhakika mkubwa, kipa Onana amekuwa akijiamini sana mpira unapokuwa kwenye miguu yake.
Na sasa takwimu zinaonyesha kwamba kipa huyo amekuwa akipiga pasi ndefu mara nyingi - baada ya kuonekana pasi fupi zimekuwa zikileta shida pindi timu inapokuwa kwenye presha ya kukabiwa juu na wapinzani.
Takwimu hizo zinaonyesha, Man United imepoteza mpira mara 142 kwenye eneo lake la ulinzi msimu huu - ikiwa ni mara sita kuzidi timu nyingine yoyote kati ya zote zilizopo kwenye Ligi Kuu England msimu huu.
Kwa mujibu wa The Athletic, kupitia takwimu za Opta ni kwamba kuna makipa watano ambao wamepiga pasi ndefu mara nyingi kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Na pasi ndefu zinazozungumzwa ni zile za mita 40, ambazo zinapigwa kwenye nafasi kwa ajili ya washambuliaji kukimbilia au wachezaji kugombea.
Kwenye pasi hizo ndefu, ni Dean Henderson pekee ndiye aliyepiga pasi chache sahihi kulinganisha na Onana, aliyekuwa na wastani wa asilimia 25.8 katika pasi ndefu 380. Kipa Onana - ambaye kwa sasa yupo kwenye rada za klabu za Saudi Arabia - alipiga pasi fupi nyingi kwenye mechi ya kwanza ya kocha Amorim kwenye timu hiyo ilipomenyana na Ipswich, Novemba mwaka jana. Na katika mechi dhidi ya Everton, Februari 22, alipiga pasi ndefu tatu tu.
Lakini, Man United ilipocheza na Arsenal, Machi 9, timu ambayo inakabia juu kuzidi Everton, kipa huyo Mcamerooni, alipiga pasi ndefu 29, ikiwa ni idadi kubwa tangu awe chini ya kocha Amorim.
Na sasa kwenye mechi tano za mwisho za Man United, Onana ameweka wastani wa pasi ndefu 20.4 - tofauti na ilivyokuwa pasi sita kwa kila mechi katika mechi za kwanza za kocha Amorim.
Baada ya beki wa kati, Lisandro Martinez kuumia, kocha Amorim amelazimika kubadilika mtindo wake wa uchezaji, huku akidai hilo linatokana na aina ya wachezaji waliopo kwenye kikosi kwa sasa.
Na mastraika wa kikosi hicho, Rasmus Hojlund na Joshua Zirkzee wamefanikiwa kuichezea asilimia 22 na 29 mtaliwa ya mipira ya juu iliyopigwa kuwaelekea wao msimu huu. Na Onana anapopiga pasi za pembeni, anayelengwa ni Alejandro Garnacho, ambaye amefanikiwa kucheza kwa asilimia tisa tu ya mipira hiyo mirefu msimu huu, ikiwa ni rekodi mbaya kabisa kwa mawinga walipo kwenye Ligi Kuu England msimu huu.