Man United, Baleba ni suala la muda tu
Muktasari:
- Mashetani Wekundu wanapanga kuifanyia marekebisho makubwa safu yao ya kiungo na kumteua kocha mkuu wa kudumu mwishoni mwa msimu.
MANCHESTER, ENGLAND: NDO hivyo. Manchester United inajiamini zaidi kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa Brighton, Carlos Baleba, dirisha la usajili wa majira ya joto.
Mashetani Wekundu wanapanga kuifanyia marekebisho makubwa safu yao ya kiungo na kumteua kocha mkuu wa kudumu mwishoni mwa msimu.
Man United hawatarajiwi kuimarisha kikosi chao dirisha la Januari chini ya kocha wa mpito Michael Carrick, ambaye atakuwa benchini kwa michezo 17 ya mwisho ya klabu msimu huu.
Kabla ya kuwasili kwa Ineos, Man United waliamua kutosajili wachezaji wapya wakati Ole Gunnar Solskjaer na Ralf Rangnick walipokuwa makocha wa muda katika madirisha ya majira ya baridi ya 2019 na 2022.
Lakini, kwa mujibu wa vyanzo vya karibu na klabu, Man United wanaanza kuwa na matumaini makubwa ya kumng’oa Baleba kutoka Amex dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kiungo huyo wa kati mwenye umri wa miaka 22 ana mkataba na Brighton hadi mwaka 2028, lakini thamani yake imeanza kushuka tangu taarifa za nia ya Man United zilipoibuka mwaka jana.
Baleba alitolewa nje ya uwanja wakati wa mapumziko ya kipindi cha kwanza mara saba msimu huu, ikiwemo mara nne na Kocha wa Brighton, Fabian Hurzeler na mara tatu akiwa na timu yake ya taifa.
Brighton walikataa ombi la Man United majira ya joto yaliyopita na makamu mwenyekiti, Paul Barber hivi karibuni alisisitiza kuwa hakuna mipango ya haraka ya kumuuza Baleba.
Thamani ya Baleba ilikadiriwa kuwa kati ya Pauni 80 milioni hadi Pauni 100 milioni, Agosti 2025 na Man United hawakuwasilisha ofa rasmi kwa kuwa tayari ilikuwa imetumia zaidi ya Pauni 200 milioni kuwasajili Bryan Mbeumo, Matheus Cunha na Benjamin Sesko.
Yeye ni mfano mwingine wa mfumo madhubuti wa usajili wa Brighton, aliletwa kama mbadala wa Moises Caicedo aliyeweka rekodi ya uhamisho kwenye Ligi Kuu England, ambaye naye alimrithi Yves Bissouma baada ya kuuzwa kwa dau kubwa kwenda Tottenham.
Huu ni mfumo uliothibitishwa kwa Brighton, kwani wamekuwa wakiwapoteza wachezaji muhimu hapo awali, kama Alexis Mac Allister aliyehamia Liverpool, lakini wengine hujitokeza na kuziba pengo.
Man United iko tayari kusajili zaidi ya kiungo mmoja majira ya kiangazi, huku nyota wengine watatu wa Ligi Kuu England wakiwa kwenye orodha yao.
Klabu inamfuatilia Elliot Anderson wa Nottingham Forest, Adam Wharton wa Crystal Palace na Alex Scott wa Bournemouth.