Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MAMBO NI MOTO! Makocha wa nusu fainali wana mizizi

MAKOCHA Pict

Muktasari:

  • Watetezi Ivory Coast wameshindwa kushikilia bomba baada ya kutolewa hatua ya robo fainali na Misri kwa mabao 3-2 na kuziacha timu hizo nne zilizotinga nusu fainali kila moja ikipambana kivyake ili kuona inaondoka na taji hilo lisilo na mwenyewe kwa sasa.

CASABLANCA, MOROCCO: FAINALI za 35 za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zinazoendelea Morocco, zimefikia patamu baada ya timu nne za mwisho kutinga nusu fainali zikisaka ubingwa wa michuano uliotemwa na Ivory Coast.

Watetezi Ivory Coast wameshindwa kushikilia bomba baada ya kutolewa hatua ya robo fainali na Misri kwa mabao 3-2 na kuziacha timu hizo nne zilizotinga nusu fainali kila moja ikipambana kivyake ili kuona inaondoka na taji hilo lisilo na mwenyewe kwa sasa.

Pape Thiaw wa Senegal ndiye kocha mwenye uzoefu mdogo zaidi kati ya makocha wanne waliopo nusu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya kufanikiwa kuing'oa Mali kwa bao 1-0.

Senegal ya Pape Thiaw itakutana na Misri ya Hossam Hassan katika mechi ya kwanza ya nusu fainali keshokutwa Jumatano, huku Nigeria ya Eric Chelle ikivaana na wenyeji Morocco wanaofundishwa na kocha wa muda mrefu, Walid Regragui.

Chelle na Regragui walikulia Ufaransa katika miaka yao ya awali, lakini dhana ya kuwa na makocha 'wa kizungu' kuifundisha timu za taifa za Afrika inaendelea kupotea taratibu.

Ingawa haijatoweka kabisa kwani timu 10 kati ya 24 zilizoshiriki AFCON 2025 Morocco zilifika na makocha kutoka Ulaya kuna mtazamo unaokua kuwa makocha wa Kiafrika wana uelewa mpana zaidi wa mchezo barani humu pamoja na uelewa wa kina wa wachezaji.

Kati ya timu zilizofika robo fainali ni Tom Saintfiet (Mali) na Vladimir Petkovic (Algeria) pekee waliokuwa na makocha wasio Waafrika.

Hata hivyo, kuna hoja kwamba kocha wa Ubelgiji, Tom Saintfiet anastahili kupewa hadhi ya 'Mwafrika wa heshima' kwa kuwa ametumia karibu miongo miwili akifundisha soka barani Afrika.

Hapa chini ni wasifu wa makocha wanne waliobaki Morocco, wote wakiwa wana mizizi ya Afrika.

MAKO 01

ERIC CHELLE (NIGERIA)

Chelle alizaliwa Ivory Coast kwa baba Mfaransa na mama raia wa Mali. Alikulia Ufaransa lakini aliwakilisha timu ya taifa ya Mali.

Akiwa mchezaji, alikuwa beki wa kati na alicheza soka lake lote nchini Ufaransa, hasa katika klabu za Valenciennes na Lens. Kama kocha, bado ni mgeni kwa kiasi fulani katika soka la Afrika.

Aliteuliwa kuifundisha Mali mwaka 2022 na alikaa madarakani kwa miaka miwili kabla ya kuondoka baada ya kufungwa na wenyeji Ivory Coast kwenye robo fainali ya AFCON iliyopita.

Uteuzi wake kuinoa Nigeria Januari 2025 ulizua mshangao, hasa baada ya kushindwa kuipeleka timu hiyo kwenye Kombe la Dunia la Marekani, Mexico na Canada, lakini kwa sasa ameifanya Nigeria kung’ara nchini Morocco.

Akiwa na umri wa miaka 48, bado ni mchanga katika taaluma ya ukocha, lakini ana nafasi ya kuandika historia na Super Eagles.

MAKO 02

HOSSAM HASSAN (MISRI)

Mshambuliaji nguli barani Afrika, Hassan ni mshindi mara tatu wa Kombe la Mataifa ya Afrika akiwa mchezaji katika kipindi cha miaka 20 kati ya 1986 na 2006.

Urefu wa maisha yake ya soka unaonekana kupitia mechi 177 alizocheza kimataifa, huku akitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Misri mara 13, akizichezea klabu zenye upinzani mkubwa pale Cairo, Al Ahly na Zamalek.

Mabao yake 69 kwa timu ya taifa bado ni rekodi ya Misri, ingawa inatarajiwa kuvunjwa hivi karibuni na Mohamed Salah ambaye ana mabao 67, jambo ambalo Hassan anatamani litokee katika mashindano haya.

Kazi yake ya ukocha haijafanikiwa sana hadi sasa, lakini nusu fainali hii ni fursa ya kubadilisha hilo. Baada ya kuiongoza Misri kufuzu Kombe la Dunia mwaka huu, sasa analenga pia kulitwaa taji la Afrika.

Anajulikana kwa hasira na ukali wake, lakini akiwa na umri wa miaka 59 amepunguza kasi hiyo, huku akiwa na ndugu yake pacha Ibrahim Hassan kama mkurugenzi wa ufundi wa timu ya taifa.

MAKO 03

WALID REGRAGUI (MOROCCO)

Kocha atakayekumbukwa daima kwa kuipeleka Morocco hadi nusu fainali ya Kombe la Dunia 2022, Regragui sasa ana nafasi ya kuimarisha urithi wake kwa kulitwaa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo baada ya miaka 50.

Hata hivyo, si kipenzi cha kila mtu nchini Morocco, kwani baadhi ya wakosoaji wanaamini hashawishi vyema vipaji alivyovikuta, ingawa tathmini hiyo inaonekana kutomtendea haki.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 50 alizaliwa Ufaransa na alikuwa beki wa kulia, akiichezea timu ya taifa ya Morocco mara 44 kati ya 2001 na 2009.

Aliwahi kuwa mshindi wa pili AFCON mwaka 2004 akiwa mchezaji, jambo linalompa motisha ya kutaka kufanya vizuri zaidi safari hii.

Ukiacha kipindi kifupi alichofanya kazi nchini Qatar, uzoefu wake wote wa ukocha umetokana na klabu za Morocco, ikiwamo miaka sita ndani ya FUS Rabat.

Pia aliiongoza Wydad Casablanca kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kuteuliwa kuwa kocha wa taifa Agosti 2022, muda mfupi kabla ya Kombe la Dunia la Qatar.

MAKO 04

PAPE THIAW (SENEGAL)

Kocha kijana zaidi na mwenye uzoefu mdogo kati ya wanne waliopo nusu fainali, Thiaw tayari ameonja mafanikio barani Afrika baada ya kuiongoza Senegal kutwaa ubingwa wa CHAN mwaka 2022, mashindano yanayohusisha wachezaji wa ligi za ndani pekee.

Alizaliwa Dakar, lakini alicheza soka lake katika klabu mbalimbali barani Ulaya, zikiwamo za Ufaransa, Uswisi, Hispania na Urusi.

Alikuwa na muda mfupi, lakini mzuri katika timu ya taifa, akifunga mabao matano katika mechi 16 kati ya 2001 na 2003 na alikuwa sehemu ya kikosi kilichofika robo fainali ya Kombe la Dunia 2002.

Aliwahi kuinoa klabu ya Niarry Tally kwa miaka mitatu nchini Senegal kabla ya kupewa jukumu la kuifundisha timu ya taifa ya CHAN.

Alirithi mikoba ya kocha nguli Aliou Cisse Desemba 2024 na ameiongoza Senegal kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika baadaye mwaka huu.

Badala ya kusaka kocha maarufu kutoka Ulaya licha ya kuvutia kocha wengi kutokana na ubora wa kikosi,  Senegal ilichagua kocha wa ndani, na uamuzi huo umeanza kuzaa matunda.