Majeraha yazidi kuitafuna Spurs
Muktasari:
- Spurs yenye maskani yao jijini London sasa ipo kwenye taharuki juu ya kuumia kwa staa huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye alilazimika kubadilishwa katikati ya kipindi cha kwanza baada ya kuumia nyama za nyuma ya paja.
LONDON, ENGLAND: TATIZO la majeruhi katika kikosi cha Tottenham Hotspur limezidi kuwa baya zaidi baada ya mchezaji wao wa kimataifa wa Brazil, Richarlison, kuondoka Uwanjani akiwa anachechemea katika mechi yao ya raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Aston Villa Jumamosi jioni.
Spurs yenye maskani yao jijini London sasa ipo kwenye taharuki juu ya kuumia kwa staa huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye alilazimika kubadilishwa katikati ya kipindi cha kwanza baada ya kuumia nyama za nyuma ya paja.
Baada ya kuanza mechi ya Ligi Kuu ya England ya Jumatano dhidi ya Bournemouth akitokea benchi, Richarlison alirudi kwenye kikosi cha kwanza katika mechi hiyo ya FA dhidi ya Villa iliyomalizika kwa kupoteza kwa mabao 2-1.
aata hivyo, kurejea kwake hakukuwa na bahati nzuri baada ya kiungo wa Villa, Muargentina, Emi Buendia, kuipatia timu yake bao la kuongoza baada ya dakika 22 tu.
Haikuishia hapo dakika chache baadae Richarlison, alianguka na kuanza kuugulia maumivu ya paja.
Baada ya kupokea matibabu kutoka kwa wataalamu wa Tottenham, mshambuliaji huyo hakuweza kuendelea na baadaye badilishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Randal Kolo Muani, ambaye alikua ameanzia benchi mechi dhidi ya Bournemouth.
Hadi sasa Spurs haijatoa taarifa rasmi juu ya ukubwa wa jeraha ambalo Richarlison amelipata ingawa ripoti za ndani zinaeleza huenda akakaa nje kwa zaidi ya mwezi.
Hiyo itamweka katika wakati mgumu kocha wa Spurs, Thomas Frank ambaye timu yake haijaanza vizuri msimu huu na moja kati ya mambo yaliyokuwa yanachangia hali hiyo ni majeraha kwa wachezaji wake muhimu.
Akizungumza baada ya kufunga bao la ushindi katika mechi hiyo iliyopigwa wikiendi iliyopia, kiungo wa raia wa England, Rogers, alisem:"Tulicheza vizuri katika nusu ya kwanza, nusu ya pili walituzidi kidogo. Tulilazimika kutoa kila kitu na nadhani tulistahili ushindi."