Majeraha ya misuli ya paja yatawala UEFA EURO

Muktasari:
FAINALI za Mataifa ya Ulaya (UEFA Euro) 2020 zimezidi kunoga baada ya kushuhudiwa nchi maarufu katika soka zikitolewa katika hatua ya 16-Bora ikiwamo nchi ya Ufaransa na Ureno ambazo zimeshindwa kuingia robo fainali.
FAINALI za Mataifa ya Ulaya (UEFA Euro) 2020 zimezidi kunoga baada ya kushuhudiwa nchi maarufu katika soka zikitolewa katika hatua ya 16-Bora ikiwamo nchi ya Ufaransa na Ureno ambazo zimeshindwa kuingia robo fainali.
Katika mashindano haya wapo wanasoka kadhaa ambao hawakuweza kushiriki michuano hiyo kutokana na majeraha waliyonayo. Wengi wao wakiwa wamepata majeraha ya misuli ya paja.
Aina hii ya majeraha ya tishu laini ndiyo yametawala katika mashindano haya na kusababisha mchezaji kama Kelvin de Bruyne wa Ubelgiji kutoka katika mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Ureno.
Kwa asilimia kubwa wengi wanaonekana kupata tatizo la kuchanika misuli ya nyuma ya paja kitabibu inajulikana kama Hamstrings Muscles.
Tatizo la kuchanika misuli ya nyuma ya paja ni moja ya majeraha yanayoongoza kuwapata wachezaji wa soka hasa wale wanaocheza ligi za kulipwa zenye ushindani mkubwa.
Tatizo hili mara nyingi huwa si mpaka mchezaji achezewe faulo bali hujikuta mwenyewe akiwa katika kasi hupata maumivu ya kuchomwa kama na kitu chenye ncha kali nyuma ya paja.
Kwa mujibu wa mtandao wa physioroom inayoripoti taarifa za wachezaji majeruhi wa soka karibu 80% ya wanasoka walio majeruhi, majeraha waliyopata ni kuchanika kwa misuli ya paja.
Si jambo la kushangaza kwa wachezaji wa mpira wa miguu kupata tatizo hili mara kwa mara kwani wao wanatumia zaidi miguu kucheza ikiwamo kupiga mashuti, kukimbia, kuruka, kukwatuliwa na kukwatua.
Mambo haya yote yanafanyika katika eneo la miguuni na nguvu kubwa inatoka katika misuli iliyopo eneo hili ikiwamo misuli ya nyuma ya paja.
Nyuma ya paja kuna misuli mikubwa mitatu inayoshirikiana kufanya kazi mbalimbali ikiwamo kurudisha paja nyuma na kupiga teke au kupiga mpira.
Misuli inapotumika sana au kuzidiwa uwezo wake huweza kupata mchoko mkali na kuwa dhaifu.
Wakati wa kucheza nako kuna kuchezewa faulo ambazo mara nyingi husababisha majeraha madogo mpaka makubwa. Wachezaji wa soka wanakumbana na faulo nyingi hasa kwa viungo na washambuliaji.
Mambo yote haya huweza kuchangia kujijeruhi ndani kwa ndani kwa misuli na na kurundika vijeraha vidogo vidogo na kuifanya misuli hii kuwa dhaifu.
Baadaye ghafla unapotumia nguvu kupita kiasi ikiwamo kutaka kuchomoka kasi misuli hii hupata shinikizo kubwa na huweza kusababisha kuchanika misuli hii.
Nyuzi nyuzi ndogo za misuli zilizo kama ‘raba band’ huweza kukunjuka kupita kiwango chake hivyo kukatika.
Mchezaji anapokimbia kwa kasi mbio fupi kama vile za mita 100, misuli hii ndio inayoirudisha miguu nyuma huku akikanyagia na vidole gumba ili kuchochea kasi zaidi.
Wakati misuli hii ikifanya kazi hii hujikuta ikielemewa na uzito wote wa mwili, wakati huo huo huwa na kazi ya hujirefusha na kujifupisha ili kwenda kasi na hapo ndipo pia misuli hupata madhara.
Yapo mambo mbalimbali yanayoweza kumweka mwanamichezo katika hatari ya kupata tatizo la kuchanika misuli ya paja.
Misuli iliyojibana iko katika hatari ya kupata tatizo hili, hii inawakumba wanamichezo wasiopasha kabla ya mazoezi au mechi.
Kama kundi la misuli litakuwa imara zaidi ya misuli pinzani (mfano misuli ya nyuma misuli inayopingana nayo huwa ni ya nyuma) kutowiana huku kunaweza kusababisha mchosho wa misuli, mara nyingi hutokea kwa misuli ya nyuma ya paja.
Misuli ya mbele ya paja huwa imara na nguvu zaidi, wakati wa michezo inayohusisha kukimbia kasi misuli ya nyuma huchoshwa mapema na kutokuwa na nguvu kuliko misuli ya mbele. Mchoko huu huweza kuleta vijeraha katika misuli.
Kama misuli hii kiasili itakuwa ni dhaifu basi nayo inakuwa haina uwezo wa kuhimili mazoezi magumu hivyo inakuwa rahisi kujeruhi.
Uwepo wa Mchoko hupunguza uwezo wa misuli kupata nishati na kuwa na nguvu hivyo nayo hukuweka katika hatari ya majeruhi.
Wanamichezo ambao bado wanaendelea kukua kimwili wako katika hatari ya kuchanika kwa misuli kwani misuli yao na mifupa haikui katika uwiano sawa kwa muda na kasi.
Urukaji wa ghafla, kujinyoosha au mgongano wowote huweza kuivuta kupita kiwango chake na hivyo kuchana misuli iliyojipachika juu ya mfupi hiyo.
Dalili ya mara kwa mara ni pamoja na mwanamichezo kujigundua kuwa na maumivu makali yanayochoma na kuuma nyuma ya paja hasa baada ya kuchoma kasi.
Hii itamfanya kusimama haraka na akiegemea mguu ulio mzima kiafya huku akishika nyuma ya paja baadaye maumivu yakizidi hukaa chini.
Ili kupunguza majeraha haya ya misuli ya paja ni vizuri wanasoka kuzingatia mazoezi mepesi ya viungo ikiwamo ya kunyoosha viungo vya mwili na kupasha moto mwili kabla na baada ya kushiriki michezo.
Usingaji (massage) wa misuli ya mapaja baada ya mechi au mazoezi magumu ni moja ya njia ambazo inatumiwa sana na wanasoka wa kimataifa kukabiliana na majeraha ya misuli.
Matumizi ya protini ya ziada na ulaji wa vyakula vyenye protini ni moja ya njia rahisi ili kukabiliana na majeraha ya misuli kwa wanamichezo.
Ukiacha ulaji protini, wachezaji wanatakiwa kunywa maji mengi angalau lita 2-3 kabla na baada ya mechi au mazoezi.
Wachezaji wanatakiwa kuepuka kucheza wakiwa wana mejaraha au kabla ya kupona vizuri.
Tathmini ya kina ya kitabibu inahitajika kwa ajili ya wachezaji wanaopona baada ya kuwa majeruhi.
Benchi la ufundi linatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na ushauri wa wataalam wa mazoezi kwani sababu nyingine ya wachezaji kupata majeraha haya ni kufanyishwa mazoezi mazito kupita kiwango.
Wachezaji wazingatie mbinu za kiuchezaji wanazopewa na wataalam wa mazoezi ya mwili na afya ili kupunguza hatari ya kupata majeraha ya misuli.
Imeandikwa na DK SHITA SAMWEL