Magalhaes awekewa pesa Arsenal kisa Al Nassr

Muktasari:
- Staa huyu anahusishwa na timu mbalimbali za Saudi Arabia ambazo zimepanga kutuma ofa kwa ajili ya kumsajili na moja kati ya hizo ni Al Nassr.
ARSENAL iko tayari kumpa ofa ya mkataba mpya beki wake wa kati na timu ya taifa ya Brazil, Gabriel Magalhaes mwenye umri wa miaka 27, ili kumzuia asiondoke katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Staa huyu anahusishwa na timu mbalimbali za Saudi Arabia ambazo zimepanga kutuma ofa kwa ajili ya kumsajili na moja kati ya hizo ni Al Nassr.
Arsenal haina mpango wa kumuuza staa huyu licha ya ofa nono ambazo zinadaiwa kuwekwa mezani na timu hizo za Saudia na ndio maana inajaribu kutaka kumsainisha mkataba mpya wakati ule wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwaka 2027. Gabriel amecheza mechi 41 na kufunga mabao manne, asisti moja.
Cristian Romero
ATLETICO Madrid wanapanga kumsajili beki wa kati wa Tottenham na Argentina mwenye umri wa miaka 26, Cristian Romero katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Romero ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027, msimu huu amecheza mechi 17 za michuano yote na kufunga bao moja.
Staa huyu amewahi kupita katika klabu za Juventus, Atalanta na Genoa.
Harry Maguire
MABOSI wa Manchester United watasubiri hadi watakapomuuza beki wao Harry Maguire kabla ya kumsajili beki wa kati wa Everton, Jarrad Branthwaite ambaye imekuwa ikihusishwa naye tangu katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Mkataba wa sasa wa Maguire unatarajiwa kumalizika mwakani.
Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana alikataa kuondoka licha ya timu mbalimbali kuhitaji saini yake,
William Saliba
REAL Madrid bado ina mpango wa kutaka kumsajili beki wa Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, William Saliba, 24, ambaye imekuwa ikihusishwa naye tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi.
Saliba ambaye mara kadhaa alizohojiwa amekuwa akisisitiza kwamba hana mpango wa kuondoka Arsenal, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Jorrel Hato
ARSENAL imengia katika vita dhidi ya Liverpool kwa ajili ya kumsajili beki kisiki wa Ajax na timu ya taifa ya Uholanzi, Jorrel Hato, 19, katika dirisha lijalo.
Hato ambaye tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 42 za michuano yote, anaonekana kuwa mmoja kati ya wachezaji vijana wanaoweza kuwa tegemeo kwa Ajax kwa miaka ijayo lakini timu hiyo ipo tayari kumuuza kwa Pauni 40 milioni.
Lookman
ATALANTA inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 50 milioni ili kumuuza mshambuliaji wao raia wa Nigeria, Ademola Lookman, 27, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Staa huyu anayewindwa na Manchester United na Newcastle United, anahusishwa sana kuondoka mwisho wa msimu kwa sababu ya kutopata nafasi ya kutosha kwenye mechi kadhaa za wiki zilizopita.
Boubacar Kamara
ASTON Villa wameshaanza mazungumzo na kiungo wao raia wa Ufaransa, Boubacar Kamara, mwenye umri wa miaka 25, kuhusu mchakato wa kumsainisha mkataba mpya. Msimu huu, Kamara hajapata muda mwingi wa kucheza kutokana majeraha ya mara kwa mara yanayomsumbua. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.
Francisco Trincao
MANCHESTER United, Newcastle na Arsenal zinapewa nafasi kubwa ya kumsajili winga wa Sporting Lisbon na Ureno, Francisco Trincao, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Awali, ilionekana anaweza kurejea Barcelona kutokana na kipengele cha mkataba wa mauziano uliosainiwa kati ya Barca na Sporting.