Madrid yataka saini ya Mainoo
Muktasari:
- Mainoo, 20, aliibukia na kuonyesha kiwango bora kabisa katika kikosi cha Man United wakati ilipokuwa chini ya kocha, Erik ten Hag.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imeripotiwa kuingia kwenye mbio za kunasa huduma ya kiungo anayetaka kuachana na Manchester United, Kobbie Mainoo.
Mainoo, 20, aliibukia na kuonyesha kiwango bora kabisa katika kikosi cha Man United wakati ilipokuwa chini ya kocha, Erik ten Hag.
Lakini, licha ya kuwa na kipaji kikubwa na matumaini makubwa ya kuwa mchezaji wa kiwango bora kwa miaka ya baadaye, Man United bado inataka kumpiga bei ili kupata pesa za kuweka sawa vitabu vya hesabu za kifedha.
Mahasimu wa Man United kwenye Ligi Kuu England, Chelsea kwa muda mrefu wameonyesha dhamira ya kutaka saini ya kiungo huyo Mwingereza.
Na sasa taarifa mpya zinafichua, miamba ya soka ya Ulaya, Real Madrid nayo imeingia kwenye mchakato wa kunasa huduma ya staa huyo wa Old Trafford.
Mahasimu wa Real Madrid huko kwenye La Liga, Atletico Madrid nao wameripotiwa kuhitaji saini ya Mainoo, ambaye amepoteza nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Ruben Amorim.
Lakini, klabu hizo mbili za La Liga zinahitaji saini ya Mainoo kwa mkopo. Kinachoripotiwa Mainoo anasakwa na timu nyingi sana, zisizopungua 10. Tangu aliporudi uwanjani kutoka kwenye majeraha ya misuli Aprili mwaka huu, Mainoo ametumika kwa dakika 90 mara mbili tu na hilo limedaiwa kumkasirisha hasa baada ya kupoteza nafasi katika kikosi cha kwanza cha Man United.
Kocha Amorim alisema: "Wazo letu siku zote ni kuwabakiza wachezaji wetu bora ili kujenga hii klabu. Lakini, tunafahamu hali ya klabu ilivyo. Ngoja tuone. Nawapenda sana wachezaji wangu, hasa wale wanaotokea kwenye akademia."
Alipoulizwa kuhusu Mainoo, Amorim alisema: "Wachezaji wangu siku zote ndio kipaumbele changu, nawapenda sana. Nataka kubaki na wachezaji wangu, hasa wale wenye vipaji vikubwa. Nina furaha na Kobbie."