Madrid yamkataza Trent kutumia gari lake

Muktasari:
- Beki huyo alisababisha minyukano miongoni mwa mashabiki wa Liverpool alipofichua kwamba atahama kwenda Hispania, na hapo awali ilionekana ataondoka bila ada baada ya kukaa miaka 20 katika timu hiyo.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid imemkataza Trent Alexander-Arnold kupeleka Hispania gari yake ya kifahari baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea Liverpool.
Beki huyo alisababisha minyukano miongoni mwa mashabiki wa Liverpool alipofichua kwamba atahama kwenda Hispania, na hapo awali ilionekana ataondoka bila ada baada ya kukaa miaka 20 katika timu hiyo.
Hata hivyo, baadaye Majogoo wa Anfield walipata ada kubwa ya Pauni 10 milioni kutoka Real Madrid kwa ajili ya Trent kujiunga mapema ili awahi kucheza Kombe la Dunia la Klabu.
Trent amesaini mkataba wa miaka sita Santiago Bernabeu, ambao ulianza Jumapili wakati dirisha la uhamisho lilipofunguliwa.
Lakini kuna jambo moja kutoka nyumbani ambalo hataweza kulipeleka kwenye timu yake mpya linalohusisha gari yake aina ya Range Rover yenye thamani ya Pauni 130,000 aliyokuwa akiendesha England. Hii ni kwa sababu Real Madrid ina mkataba wa udhamini na BMW ambao unazuia wachezaji kuendesha magari mengine yoyote katika uwanja wa mazoezi wa klabu.
BMW huwa inawapa wachezaji wa Real Madrid magari ya kutumia msimu mzima ili kuwazuia kutumia ndinga za kampuni nyingine.
Mkataba huo unajumuisha wachezaji kupewa magari ya umeme na mafuta, na wachezaji kama Kylian Mbappe na Jude Bellingham walichagua BMW XM ambayo inagharimu karibu Pauni 152,000, lakini huwa inatolewa bure.
Kulingana na taarifa ya Fabrizio Romano, gwiji wa habari za usajili Ulaya, ada ya uhamisho ya kuvunja mkataba wa Trent itakuwa ni Euro 1 bilioni. Kiasi hicho kikubwa kinamaanisha klabu yoyote inayotaka kumchukua mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 kutoka Bernabeu siku za usoni itahitaji kulipa zaidi ya mara nne ya rekodi ya sasa ya uhamisho.