Madrid, Trent ishu yao iko hivi

Muktasari:
- Beki huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 26, amekubali mkataba wa miaka mitano, ambao utamfanya awe analipwa Pauni 240,000 kwa wiki wakati atakapotua kwenye kikosi cha Los Blancos wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
MADRID, HISPANIA: REAL Madrid inataka kufanya fasta kwenye usajili wa beki wa kulia wa Liverpool, Trent Alexander-Arnold ili inase huduma yake kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia la klabu.
Beki huyo Mwingereza mwenye umri wa miaka 26, amekubali mkataba wa miaka mitano, ambao utamfanya awe analipwa Pauni 240,000 kwa wiki wakati atakapotua kwenye kikosi cha Los Blancos wakati wa dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Mkataba wa Alexander-Arnold huko Anfield utafika ukomo Juni 30 - lakini michuano ya Kombe la Dunia la klabu litaanza Juni 15. Kutokana na hilo, Real Madrid sasa ipo tayari kulipa ada, kiasi cha Pauni 5 milioni ili kumsajili beki huyo Juni 1, aweze kuungana na wenzake akiwamo Jude Bellingham kwenye msafara wa kwenda Marekani inakofanyika michuano hiyo. Madrid ilionyesha dhamira ya kumnasa beki huyo tangu kwenye dirisha lililopita la Januari, lakini mabosi wa Liverpool waligoma kumruhusu nahodha wao msaidizi aondoke, ili kumsaidia kocha Arne Slot kunasa ubingwa wa Ligi Kuu England kwenye msimu wake wa kwanza.
Kocha Mdachi Slot hakutaka kumruhusu beki huyo aondoke kutokana na kuwa na macha-guo machache kwenye kikosi, lakini sasa mchezaji mwenyewe ni majeruhi hivyo Liverpool hawawezi kupoteza fursa ya kupata pesa.
Liverpool bado kijasho kinawatoka juu ya uamuzi wa mikataba mipya ya mastaa wake wengine Mohamed Salah na Virgil van Dijk, ambao pia mikataba yao itafika tamati Juni 30.