MACHOZI: Ronaldo amlilia mwamuzi wa Clasicco

Muktasari:
- Mwamuzi huyo alitoa penalti tatu na kadi nyekundu moja kwa beki Sergio Ramos wa Madrid baada ya kumkwatua Neymar wakati akielekea kumwona mlinda mlango, Victor Valdes
MADRID, HISPANIA
BAADA ya kukubali kipigo cha mabao 4-3 katika dimba lao la Santiago Bernabeu, staa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo, ameamua kumshambulia mwamuzi wa pambano hilo, Alberto Undiano Mallenco.
Mwamuzi huyo alitoa penalti tatu na kadi nyekundu moja kwa beki Sergio Ramos wa Madrid baada ya kumkwatua Neymar wakati akielekea kumwona mlinda mlango, Victor Valdes.
Hakuna alichofanya Ronaldo baada ya mechi hiyo zaidi ya kumlaumu Mallencon kutokana na penalti mbili alizowapa Barcelona pamoja na kadi nyekundu ya Ramos, huku hasimu wake, Lionel Messi akipiga ‘Hat Trick’.
“Tuna huzuni kwa sababu tulistahili makubwa, lakini mapambano yanaendelea. Ilikuwa ngumu kwa sababu watu wengi hawakutaka sisi tushinde kwa sababu Barcelona ingekuwa imeondoka katika mbio,” alisema Ronaldo.
“Labda hawataki Real Madrid ichukue La Liga. Nimekuwa hapa kwa miaka mitano, najua mambo mengi yalivyo na nina matumaini tutashinda bila ya kujali hilo. Nasikia huzuni kwa sababu baada ya kuongoza kwa 3-2 na kumiliki mchezo, mwamuzi alifanya maamuzi ya kustaajabisha.”
Undiano Mallenco alichezesha katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, ana uzoefu pia wa kuchezesha mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya na amewahi kuchaguliwa kuwa Mwamuzi Bora wa Hispania mwaka 2005 na 2007.
Lakini Ronaldo amemshutumu kwa kuwa na wasiwasi katika uamuzi wake kwenye pambano la juzi Jumapili la El Clasicco.
“Kulikuwa na makosa mengi ndani ya mechi moja. Katika mechi ya Real Madrid na Barcelona inabidi uwe na mwamuzi ambaye yuko juu ya mechi. Sitaki kutoa visingizio lakini kama utatazama tena dakika 90 za mechi mwamuzi alifanya makosa mengi,” alisema.
“Nadhani hakuwa mwamuzi wa hadhi ya mechi hii. Nilimtazama na alionekana kutojielewa. Ni kwa sababu alikuwa na wasiwasi na kuwa na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi. Real Madrid ni klabu kubwa zaidi duniani na hilo linasababisha kuwe na wivu mwingi juu yao.”
Kocha wa Barcelona, Gerardo Martino, amekiri kwamba kutokana na ushindi huo, wamerudi katika mbio za ubingwa msimu huu huku wakiwa na pointi 69 nyuma ya Atletico Madrid na Real Madrid. “La Liga haijaisha. Hatutaacha kupambana na matokeo haya yameturudisha katika mbio. Hii ni nafasi yetu ya mwisho. Hatutaki kuachwa tena.”