Calvert-Lewin atua anga za kocha Man United

Muktasari:
- Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 yupo huru baada ya kuondoka Everton kufuatia kumalizika kwa mkataba wake wiki hii.
MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER UNITED inafanya jaribio la kushangaza kumsajili mchezaji huru Dominic Calvert-Lewin ambaye msimu uliopita aliichezea Everton.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 yupo huru baada ya kuondoka Everton kufuatia kumalizika kwa mkataba wake wiki hii.
Kocha wa Man United, Ruben Amorim anataka kumsajili haraka Calvert-Lewin wakati viongozi wa timu wakihangaika kusawazisha bajeti yao.
Vyanzo vya ndani vimefichua kuwa Man United tayari imewasiliana na wakala wa mshambuliaji huyo kuulizia kama anaweza kujiunga na Mashetani Wekundu.
Hadi sasa United imeshamalizana na mshambuliaji wa Wolves, Matheus Cunha kwa dau la pauni 62.5 milioni pia inapambana kufanikisha dili la mshambuliaji wa Brentford, Bryan Mbeumo.
Vilevile kocha Amorim pia anataka kuwauza baadhi ya washambuliaji wake ambapo Rasmus Hojlund, Marcus Rashford, Alejandro Garnacho, Jadon Sancho na Antony wote wako hatarini kuondoka.
Man United imeshatuma ofa mbili kwa Mbeumo lakini Brentford bado imeshikilia msimamo wake kutaka kiasi cha pauni 65 milioni kwa staa huyo raia wa Cameroon.
Wakati huo huo, Juventus iko tayari kuipa Man United kiungo wa zamani wa Aston Villa, Douglas Luiz kama sehemu ya dili la kumsajili Sancho, ambaye alitolewa kwa mkopo Chelsea msimu uliopita.
Sancho ni miongoni mwa wachezaji watano ambao Amorim amewaambia wasihudhurie mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya yanayoanza leo huko Carrington, kwani hawako katika mipango yake.
Ijumaa ya wiki iliyopita, Man United ilithibitisha kuwa Sancho, Rashford, Garnacho, Antony na Tyrell Malacia wote wanataka kuondoka Old Trafford.