Machalii wa kutazamwa EPL msimu wa 2023-2024

LONDON, ENGLAND. IMEBAKI mwezi mmoja msimu wa Ligi Kuu England 2023-2024 uanze huku timu zikiendelea na maandalizi zingine zikicheza mechi za kirafiki.
Wakati mashabiki macho yao yapo kwa mastaa wapya ambao wamesajiliwa kwenye dirisha hili la usajili la kiangazi, akili za makocha zipo kwa wachezaji wao ambao wanajifua na matizi ya kufa mtu. Aidha huu ni wakati wa wachezaji makinda kuwashawishi makocha kupitia maandalizi haya ya msimu mpya.
Ingawa itakuwa ngumu sana lakini vipaji vyao ndio vina nafasi kubwa ya kuwashawishi makocha kupitia mechi za kirafiki ambazo ni sehemu ya kujiweka fiti.
Hawa hapa makinda watano ambao huenda wakatoboa kikosi cha kwanza kutokana na vipaji vyao vya kucheza soka na wamejumuishwa kwenye maandalizi ya msimu mpya.
Arsenal – Reuell Walters
Arsenal ilitinga fainali ya Kombe la FA kwa upande wa vijana chini ya kocha Jack Wilshere msimu uliopita. Ingawa walifungwa mabao 5-1 dhidi ya West Ham lakini kikosi chao kilikuwa na makinda hatari akiwemo kinda huyo. Mikel Arteta ameshuhudia kipaji chake kinda huyo mwenye umri wa miaka 18- aliwahi kucheza kikosi cha kwanza akitokea benchi msimu uliopita. Sasa baada ya Arteta kumuamini huenda akapata nafasi za kucheza kikosi cha kwanza msimu ujao.
Chelsea – Andrey Santos
Chelsea ilimsajili kinda huyo kutokea Vasco da Gama tangu dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu. Lakini kutokana na ujio wa Enzo Fernandez kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 alibaki Brazil akicheza kwa mkopo huku akishughulikia kibali cha kufanya kazi England. Kiungo huyo anakipaji cha kucheza na huenda akapewa nafasi na Mauricio Pochettino. Chelsea ina makinda wengi wenye vipaji kama Levi Colwill (20) ambaye alikipiha Brighton kwa mkopo, na Lewis Hall (18).
Liverpool – Ben Doak
Beki huyo mwenye umri wa miaka 20 alikuwa Bolton akikipiga kwa mkopo Bolton msimu uliopita. Baada ya kurejea Liverpool anatarajia kuungana na wachezaji wenzake wa kikosi cha kwanza msimu ujao. Lakini itakuwa ngumu kupenya kikosi kutokana na uwepo wa Trent Alexander-Arnold. Beki huyo alijiunga na Liverpool akitokea Celtic mwaka 2022. Ana rekodi ya kufunga mabao matano na akatengeneza asisti mbili katika mechi 14 za timu ya vijana. Kwa mujibu wa ripoti Jurgen Klopp anamkubali kinda huyo mwenye umri wa miaka 17.
Manchester United – Kobbie Mainoo
Mashabiki wana matarajio makubwa baada ya Amad kukiwasha msimu uliopita alipokuwa Sunderland kwa mkopo. Nyota huyo alifunga mabao 14 na kutengeneza asisti nne. Sasa macho ya mashabiki yapo kwa kiungo kinda mwenye umri wa miaka 18, Kobbie Maino. Erik ten Hag alimpa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara tatu msimu uliopita. Pia ni miongoni mwa makinda ambao wapo kwenye kikosi kinachojiandaa na msimu mpya.
Manchester City – Oscar Bobb
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19 alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wenye umri wa miaka 21 misimu miwili mfululizo. Winga huyo alifunga mabao nane na akatengeneza asisti 18 kwenye kikosi cha vijana cha Man City. Kinda huyo huenda akapewa nafasi endapo Cole Palmer akitolewa kwa mkopo katoka dirisha hili la kiangazi. Aidha kwa vile Bernardo Silva na Riyad Mahrez wana hatihati ya kuondoka basi huenda akapewa nafasi.