Arsenal, Chelsea vuta nikuvute kwa Sesko

Muktasari:
- Arsenal bado haijafanya uamuzi wa mwisho juu ya mshambuliaji huyo, baada ya kumweka Sesko kwenye orodha ya mastraika inayowataka dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya, lakini huku ikimtaka pia Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon.
LONDON, ENGLAND: KUMEANZA kuchangamka. Ndicho unachoweza kusema baada ya Chelsea na Arsenal kuhamishia vita ya London derby kwenye usajili wa straika, Benjamin Sesko kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi.
Arsenal bado haijafanya uamuzi wa mwisho juu ya mshambuliaji huyo, baada ya kumweka Sesko kwenye orodha ya mastraika inayowataka dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya, lakini huku ikimtaka pia Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon.
Kikosi hicho cha Arsenal kinachonolewa na Mhispaniola, Mikel Arteta kinafahamu wazi kinahitaji huduma ya mshambuliaji wa kati dirisha hili ili kwenda kuboresha safu hiyo baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England kwa misimu mitatu mfululilizo na kukomea kwenye nusu fainali katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
Imekuwa ikimfukuzia straika Sesko kwa muda sasa baada ya kukaribia kumsajili mwaka jana na mwaka huu ilionekana kuweka nguvu kwenye usajili wa mkali hyo wa RB Leipzig. Chelsea, tayari imeshasajili straika kwenye dirisha hili, ilipoibwaga Manchester United kwenye dili la Pauni 30 milioni la kumnasa Liam Delap kutoka Ipswich Town.
Hata hivyo, Chelsea bado haijamaliza kwenye ishu ya mastraika na ndiyo maana inahitaji huduma ya Sesko na kuvamia mawindo ya Arsenal.
The Blues imemweka Sesko kwenye mipango yao, lakini pia ikimsaka Hugo Ekitike, ambaye anaripotiwa mazungumzo na klabu ya Eintracht Frankfurt yamefikia kwenye hatua nzuri, kumsajili kwa Pauni 84 milioni.
Gharama za kumpata Ekitike inaweza kuwafanya kuhamia kwa Sesko, ambaye Pauni 60 milioni tu, klabu yake ya RB Leipzig itakuwa tayari kumpiga bei.
Arsenal inakabiliwa na vita nyingine kwa upande wa Gyokeres na Manchester United imeripotiwa kuhitaji saini ya mshambuliaji huyo ili akafanye kazi tena chini ya Kocha Ruben Amorim.
Arsenal haina mbadala kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi zaidi ya kunasa straika wa kiwango cha dunia baada ya msimu uliopota kuwategemea Kai Havertz na Gabriel Jesus, ambao iliiangusha timu hiyo kwenye mipango yao ya kunyakua mataji.