Lewandowski akacha timu ya taifa kisa kocha

Muktasari:
- Staa huyo wa Barcelona alisema amepoteza imani na kocha Michal Probierz baada ya kumvua kitambaa cha unahodha wa timu hiyo ya taifa ya Poland.
WARSAW, POLAND: STRAIKA gwiji, Robert Lewandowski ameamua kujiweka kando kuichezea Poland hadi hapo kocha atakapofutwa kazi.
Staa huyo wa Barcelona alisema amepoteza imani na kocha Michal Probierz baada ya kumvua kitambaa cha unahodha wa timu hiyo ya taifa ya Poland.
Lewandowski, 36, amefunga mabao 85 katika mechi 158 alizochezea timu ya taifa.
Aliposti mtandaoni: “Kutokana na hali ilivyo nimepoteza imani na kocha wa timu ya taifa ya Poland, nimeamua kujiweka pembeni kuichezea timu hiyo hadi hapo kocha atakapobadilishwa.
“Natumaini nitaweza kuichezea timu hii kwa ajili ya mashabiki bora kabisa duniani.”
Licha ya kuwa na hadhi kubwa huko kwao, baadhi ya mashabiki wa Poland wamekuwa wakimkosoa straika huyo kutokana na kukosa mechi za hivi karibuni. Kocha Probierz aliamua kumweka kando straika huyo kwa kumvua unahodha na kitambaa kukabidhiwa kiungo wa Inter Milan, Piotr Zielinski.
Lakini, Lewandowski uamuzi wake wa kustaafu soka la kimataifa umeshtua dunia. Staa huyo anatajwa kama mchezaji bora zaidi wa Poland kwenye kipindi hiki tangu alipoanza kucheza mwaka 2008.
Kwenye ngazi ya klabu, Lewandowski alishinda Bundesliga mara mbili alipokuwa Borussia Dortmund na mara nane alipokuwa akikipiga Bayern Munich, ambako pia alinyakua taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya 2020.
Baada ya hapo, Lewandowski alikwenda kunyakua mataji mawili ya LaLiga baada ya kujiunga na Barcelona miaka mitatu iliyopita.