Sakata la Dabi, Ally Kamwe aibua mambo mapya

Muktasari:
- Akizungumza jioni hii katika makao makuu ya Yanga, Kamwe amesema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi Almas Kasongo ameshindwa kufafanua vizuri matakwa manne kwamba yapo ya muda mfupi na muda mrefu.
MSEMAJI wa Yanga, Ally Kamwe amesema klabu hiyo, iko siriazi katika msimamo wa kutocheza mechi ya Kariakoo Dabi dhidi ya Simba, akisema Bodi ya Ligi Tanzania imepotosha juu ya matakwa yao manne.
Akizungumza jioni hii katika makao makuu ya Yanga, Kamwe amesema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi Almas Kasongo ameshindwa kufafanua vizuri matakwa manne kwamba yapo ya muda mfupi na muda mrefu.
Kamwe amesema matakwa ya muda mfupi ni pamoja na kuvunjwa kwa Kamati ya Usimamizi ya Ligi kwa kile ilichodai imeshindwa kusimamia kwa weledi usimamizi wa Ligi kwa msimu wa 2024/25
Amesema takwa la pili la muda mfupi ambalo linakwenda sambamba ni kujiuzulu kwa Kasongo alipotosha Bodi wakati wa kuahirishwa kwa mchezo namba 184 uliopangwa kufanyika Machi 8, 2025.
"Jambo lingine la muda mfupi ni kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, wote mnajua kumekuwa na vilio vingi juu ya maamuzi ya waamuzi, waamuzi wanafanya makosa na bado wanapewa mechi za kuamua ," amesema Kamwe.
"Kama hamfahamu hii Kamati ya waamuzi ipo chini ya Katibu Mkuu wa TFF kwa kuwa matatizo yamekuwa mengi Yanga tunasema na yeye atupishe.
Aidha, Kamwe amesema takwa la kuunda Bodi huru ndio jambo la muda mrefu ambalo wamewaachia TFF na Bodi kulifanyia kazi ambapo endapo halitafanyiwa kazi kwa uzito wanaweza wasishiriki Ligi msimu ujao.
AIBUA TUHUMA MPYA
Katika hatua nyingine Kamwe, ameibua tuhuma nzito juu ya fedha za ubingwa.
Kamwe amesema endapo Yanga haitapewa majibu sahihi juu ya fedha za ubingwa wa Kombe la Shirikisho la walilotwaa msimu uliopita hawatacheza fainali ya msimu huu.
Yanga ilichukua ubingwa huo msimu uliopita baada ya kuing'oa Azam FC kwa matuta, katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
"Nataka kuongeza, nimeona wametoa ratiba kwamba tutacheza Fainali ya Shirikisho Juni 28, sasa niseme tuwaambie waandaji wa mashindano haya na wadhamini wake kwamba kama hatutapewa fedha zetu za ubingwa hatutacheza mchezo wa fainali msimu huu.
"Tumevumilia vya kutosha, tumechoka kuandika barua kila wakati tukikumbusha kuhusu fedha hizi sasa tumeona tutoke hadharani tuyaweke wazi ili watu wajue."
Mwanaspoti ulipomtafuta, Mkurugenzi wa Sheria Habari na Masoko wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alipotafutwa na kuulizwa juu ya tuhuma hizo za Yanga alisema yupo safarini na kutaka atafutwe Katibu Mkuu, Wilfred Kidao. Juhudi za kupata viongozi wa TFF zilishindikana kwa vile hawakupokea simu zao.