Liverpool yafikiria kumpa kazi Xabi Alonso
Muktasari:
- Alonso alipigwa chini Bernabeu mapema mwezi huu, akimaliza kipindi chake cha ukocha katika kikosi hicho baada ya kukiongoza kwenye mechi 34 pekee.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL inaripotiwa kuanza mawasiliano na Xabi Alonso kuhusu uwezekano wa kwenda kuchukua nafasi ya Kocha wa Anfield, Arne Slot na inadaiwa Mhispaniola huyo ameonyesha nia ya kukubali kibarua hicho.
Alonso mwenye umri wa miaka 44 ana nia ya kurejea Merseyside baada ya kutokuwa na kazi kwa sasa kufuatia kufutwa kazi huko Real Madrid.
Alonso alipigwa chini Bernabeu mapema mwezi huu, akimaliza kipindi chake cha ukocha katika kikosi hicho baada ya kukiongoza kwenye mechi 34 pekee.
Liverpool inapanga kumpa mchongo wa kurejea kwenye kazi yake ya ukocha.
Kwa mujibu wa AS, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England wamewasiliana na Alonso huku presha ikiendelea kuongezeka kwa kocha Arne Slot.
Liverpool inataka kumteua Alonso kuanzia mwanzo wa msimu ujao na hawajaondoa uwezekano wa kufanya mabadiliko mapema zaidi.
Alonso anatamani sana kurejea Anfield, akiwa na kumbukumbu nzuri za kipindi chake akiwa mchezaji wa Liverpool.
Alishinda Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Super Cup na Community Shield akiwa na Liverpool. Pia alifunga mabao 18 na kuasisti mara 20 katika mechi 210.
Liverpool waliwasiliana na wawakilishi wa Alonso ili kupima kama angekuwa tayari kuchukua nafasi ya Slot. Viongozi wenye ushawishi mkubwa ndani ya klabu wanaamini Alonso angekubali kazi hiyo endapo angepewa nafasi, baada ya mazungumzo ya awali kuwa chanya.
Alonso aliiongoza Bayer Leverkusen kushinda taji lao la kwanza kabisa la Bundesliga mwaka 2024, jambo lililomfanya kuwa mmoja wa makocha wanaohitajika zaidi barani Ulaya.
Hatimaye alichagua kuchukua mikoba ya Carlo Ancelotti katika benchi la ufundi la Real Madrid, baada ya awali kukataa ofa kutoka Bayern Munich na Liverpool. Arne Slot, 47, yuko katika hatari ya kufutwa kazi baada ya timu yake kupokea kipigo cha 3-2 kutoka kwa Bournemouth.