Liverpool inahaha kumsajili Waldemar Anton

Muktasari:

  • Staa huyu ambaye yupo kwenye kikosi cha Ujerumani kinachoshiriki michuano ya Euro inayoendelea huko Ujerumani, kwenye mkataba wake ana kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Pauni 19 milioni.

LIVERPOOL hivi karibuni imetuma maombi ya kutaka kumsajili beki wa kati wa Stuttgart, Waldemar Anton katika dirisha hili.

Staa huyu ambaye yupo kwenye kikosi cha Ujerumani kinachoshiriki michuano ya Euro inayoendelea huko Ujerumani, kwenye mkataba wake ana kipengele kinachomruhusu kuondoka ikiwa timu inayomhitaji italipa Pauni 19 milioni.


BAADA ya Mason Greenwood, Juventus pia inahitaji saini ya winga wa Manchester United Jadon Sancho ambaye imethibitika kuwa hatorudi Man United hadi pale atakapomuomba msamaha Erik ten Hag jambo ambalo yeye hayuko tayari kulifanya. Sancho ambaye alitimkia kwa mkopo Borussia Dortmund katika dirisha lililopita la majira ya baridi, mkataba wake na Man United unamalizika mwaka 2025.


WEST Ham imevutiwa na kiwango cha mashambuliaji wa Atletico Madrid Samu Omorodion na inataka kumsajili katika dirisha hili.

Samu ambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo Alaves, alionyesha kiwango bora akifunga mabao nane kwenye mechi 21, pia amehudumu kwenye timu mbalimbali za taifa za Hispania kwa upande wa vijana kuanzia  U-19 na U-21.


KOCHA mpya wa Bayern Munich, Vincent Kompany amefanya mawasiliano na beki wa kati wa VfB Stuttgart na Japan, Hiroki Ito ili kumshawishi akubali kusaini mkataba wa kuitumikia timu ya Bayern kwa msimu ujao.

Mbali ya Hiroki, Kompany pia anahitaji huduma ya Joe Gomez kutoka Liverpool sambamba na Jonathan Tah wa RB Leipzig.


WEST Ham bado haijafikia muafaka katika mazungumzo yake na Udinese kwa ajili ya kumsajili beki wa timu hiyo, Nehuen Perez, 23, katika dirisha hili baada ya kutuma wawakilishi wake kwenda Italia ili kufanikisha mchakato wa kumsajili. Mkataba wa Nehuen unatarajiwa kumalizika mwaka 2027. Msimu uliopita alicheza mechi 36 za michuano yote.


VALENCIA tayari imeshasajili kipa mpya atakayeziba pengo la kipa wao Giorgi Mamardashvili ambaye anahusishwa na Chelsea, Bayern Munich na baadhi ya timu nyingine kubwa barani Ulaya zinazotaka kumsajili baada ya kumalizika kwa michuano ya Euro. Awali, Newcastle iliripotiwa kutaka kumsajili tangu dirisha lililopita lakini kwa sasa imeachana naye baada ya kuambiwa anauzwa kwa Euro 35 milioni.


ASTON Villa imefikia patamu kwenye mazungumzo yake na mabosi wa  Marseille kwa ajili ya kuipata huduma ya kiungo wa timu hiyo, Matteo Guendouzi, 25, katika dirisha hili. Matteo ambaye aliwahi kuichezea Arsenal kabla ya kurudi Ufaransa baada ya kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu, mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2028.