Laporta, Raphinha walalamika Barcelona
Muktasari:
- Miamba hiyo ya La Liga ilikerwa mwishoni mwa wiki baada ya Claudio Echeverri kuepuka kadi nyekundu kufuatia kile kilichoonekana kama kumkanyaga beki Jules Kounde.
BARCELONA, HISPANIA: RAIS wa Barcelona, Joan Laporta, amesema kuna njama za kuizuia klabu hiyo kushinda ligi kufuatia kile kilichotokea dhidi ya Girona.
Miamba hiyo ya La Liga ilikerwa mwishoni mwa wiki baada ya Claudio Echeverri kuepuka kadi nyekundu kufuatia kile kilichoonekana kama kumkanyaga beki Jules Kounde.
Uamuzi huo wa kutatanisha ulifuata pia maamuzi ya kutomtoa nje Giuliano Simeone katika kipigo kwenye Copa del Rey dhidi ya Atlético Madrid. Uamuzi huo uliifanya klabu kutoa taarifa ndefu ikithibitisha kuwa waliwasilisha malalamiko yao kwenda kwenye Shirikisho la soka la Hispania (RFEF) kuhusu wasiwasi mkubwa juu ya maamuzi ya mara kwa mara ya waamuzi ambayo wanaona yanaharibu mchezo na kukosa vigezo vya uthabiti.
Sasa Laporta ameongeza msisitizo kwenye malalamiko hayo, akidai kuwa kuna watu wasiotajwa ambao hawataki Barcelona ifanikiwe msimu huu, aliposema katika uzinduzi wa kampeni yake ya kuchaguliwa tena, amesema: “Tunaitetea Barca ili tufurahie mafanikio ya kimichezo. Tuna kundi la wachezaji katika vyumba vya kubadilishia nguo ambalo ni hazina, wachezaji waliokulia hapa wakiwa wameungana na vipaji kutoka sehemu nyingine za dunia, wote wakifanya vizuri chini ya Flick na Deco.
“Najua hali ilivyo kule, kazi anayofanya Flick, tabia za wachezaji na nina hakika tutashinda La Liga. Itakuwa ligi inayopiganwa dhidi ya kila kitu na kila mtu, kwa sababu hawataki tu kutushinda uwanjani. Wanataka kutushinda nje ya uwanja pia, ni wazi. Kuna wengi ambao hawataki tushinde, kuna makundi fulani yenye nguvu ambayo hayako upande wetu. Tumekuwa na ratiba ngumu ya mechi za Jumapili na Jumatano, na ni kawaida kushuka kiwango. Lakini pale tunaposhuka, wengine wanachukua fursa. Kwa mfano, tukio la kumkanyaga Kounde. Tutarejea katika ubora wetu na kuirudisha soka yetu. Nimezungumza nao na wako makini kabisa.”
Laporta si wa kwanza Camp Nou kulalamika. Winga wa Brazil, Raphinha, pia alitumia mitandao ya kijamii kupendekeza kuwa klabu pinzani zimekuwa zikinufaika na maamuzi tofauti ya waamuzi msimu huu, alipoandika: “Bado tuna mengi ya kuboresha, lakini si sisi tu. Ni vigumu sana wakati sheria zinakuwa tofauti kulingana na kama ni kwa faida yako au dhidi yako. Lakini, kama tunapaswa kucheza dhidi ya kila mtu ili tushinde, sawa tu... Tutafanikiwa. Daima Barca.”