HAKUNA NAMNA! Rashford mmoja anavyoweka ubaoni mastaa sita Barca
Muktasari:
- Staa huyo amefunga mabao 10 na kuasisti 13 na atagharimu Pauni 26 milioni, ni dili ambalo linaonekana ni la bei nafuu kabisa.
BARCELONA, HISPANIA: RAIS wa Barcelona, Joan Laporta na mkurugenzi wa michezo Deco, wanadaiwa kuwa na imani ya kwamba wanafanya uamuzi sahihi kwa kumsajili Marcus Rashford kwa mkataba wa kudumu mwishoni mwa mkopo wake wa msimu mmoja kutoka Manchester United.
Staa huyo amefunga mabao 10 na kuasisti 13 na atagharimu Pauni 26 milioni, ni dili ambalo linaonekana ni la bei nafuu kabisa.
Hata hivyo, miamba hiyo ya Catalunya inatafuta njia ya kupunguza au hata kufuta gharama hiyo kwa kutoa wachezaji kama sehemu ya makubaliano ya kubadilishana. Ripoti kutoka Hispania ilitaja majina mawili awali, lakini kwa sasa inaelezwa kuna manne zaidi yameongezeka.
Ferran Torres
Hakuna mchezaji wa Barcelona aliyefunga mabao mengi zaidi ya Torres (16) msimu huu, lakini bado amekuwa akihusishwa na kuondoka Nou Camp tangu aliposajiliwa kutoka Manchester City kwa Pauni 48 milioni, Januari 2022.
Inaelezwa Barcelona itachagua katiya Torres na Robert Lewandowski mwishoni mwa msimu. Kwa kuzingatia hali ya kifedha ya klabu, huenda ikampatia Lewandowski nyongeza ya mkataba kwa masharti kumpunguzia mshahara, huku ikimuuza Torres au kumtumia katika dili la kubadilishana na Rashford.
Kuna uwezekano mkubwa watahitaji nyongeza ya fedha kutoka Man United, ambao wangekuwa wanapata mshambuliaji wa ushindani mkubwa katika nafasi zote tatu za mbele.
Marc Casado
Kiungo mwenye umri wa miaka 22 aliyehitimu La Masia anaripotiwa kuacha mlango wazi kwa uhamisho wa kwenda Saudi Arabia majira ya kiangazi. Ripoti zinasema Barcelona wangemjumuisha Casado, anayekadiriwa kuwa na thamani ya Pauni 22 milioni na ameanza mechi 12 msimu huu katika dili la Rashford kwa kuwa wako tayari kuachana naye.
Ikiwa Man United itatumia fedha nyingi kwa kiungo mmoja kati ya Elliot Anderson, Adam Wharton au Carlos Baleba kama ilivyoripotiwa, itahitaji kiungo mwingine wa kati kwa gharama ndogo au bila kutumia fedha nyingi jambo ambalo lingetimia katika dili la kubadilishana na Rashford.
Frenkie de Jong
Inaonekana ni hadithi inayorudiwa kila dirisha la usajili. Sakata la uhamisho wake lilifikia kilele majira ya kiangazi 2022 wakati Man United walipokubali ofa na Barcelona, lakini De Jong alikataa kuondoka. Amesaini nyongeza ya mkataba hadi Oktoba 2029, hivyo chaguo hili linaonekana kama ndoto.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini nyongeza hiyo ililenga kuhakikisha ada nzuri ya uhamisho endapo klabu nyingine zitamfuata.
Ingawa ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa na kiongozi muhimu Barcelona, nafasi yake haijawahi kuonekana kuwa salama kabisa. Iwapo Man United ingetoa fedha pamoja na Rashford kwa ajili yake, Barcelona huenda ikafungua milango. Kiungo cha De Jong na Kobbie Mainoo kingeweza kuwa cha kuvutia sana.
Ronald Araujo
Wengi huenda wasingemtaja Araujo kama nahodha wa Barcelona. Beki huyo wa kati ameanza mechi saba tu za La Liga msimu huu kwa sababu ya majeraha na mapumziko ya afya ya akili.
Amehusishwa mara kwa mara katika dili za kubadilishana au kuuzwa ili kuongeza mapato. Ripoti zinasema Barcelona ingekubali kubadilishana moja kwa moja kwa Rashford. Lakini Man United tayari ina mabeki bora zaidi, hivyo hilo linaweza lisiwe chaguo la kuvutia sana.
Roony Bardghji
Bao lake la dakika ya 87 katika ushindi wa 4-3 dhidi ya Manchester United Novemba 2023 lilizua tetesi za kuhusishwa na Old Trafford.
Barcelona ilimsajili kutoka Copenhagen kwa Pauni 2 milioni tu, lakini hajapata nafasi nyingi licha ya kuonyesha kipaji kikubwa hasa kutokana na ushindani mkali upande wa kulia wa ushambuliaji Barcelona.
Kwa Man United au klabu yoyote, kupata mchezaji mwenye hata nusu ya ubora wa Lamine Yamal ni jambo la kuvutia. Akiwa na miaka 20, ana thamani kubwa ya baadaye iwapo atasajiliwa kwa bei nafuu kama sehemu ya dili la Rashford.
Eric Garcia
Baadhi ya mashabiki wa Man United wanaweza wasifurahie kubadilisha nyota wao wa akademi kwa mchezaji ambaye hakufanikiwa Manchester City, lakini Garcia ameonyesha kuwa mchezaji muhimu Barcelona akicheza beki wa kati, beki wa kulia na hata kiungo wa chini.
Thamani yake kwa sasa inaonyesha angeweza kuwa sehemu ya kubadilishana moja kwa moja na Rashford. Viongozi wa INEOS wanaweza kuona kuwa mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na uwezo wa kucheza nafasi tofauti. Akiwa na miaka 25 ni chaguo linalofaa kama mbadala.