Lamine Yamal, Bellingham nani zaidi?

Muktasari:
- Mastaa hawa ambao mmoja anacheza Barcelona na mwingine Real Madrid watakapokutana watakuwa wanakumbushia El Classico.
BERLIN, UJERUMANI: KATIKA mchezo wa fainali ya kesho kati ya England na Hispania unaotarajiwa kupigwa katika dimba la Olympiastadion, jijini Berlin kuanzia saa 4:00 usiku, miongoni mwa wachezaji wenye umri mdogo ambao wanaosubiriwa kwa hamu kuonekana nini wanafanya ni Jude Bellingham na Lamine Yamal.
Mastaa hawa ambao mmoja anacheza Barcelona na mwingine Real Madrid watakapokutana watakuwa wanakumbushia El Classico.
Hapa tumekuletea data zao kamili katika michuano kuanzia ilipoanza hadi sasa.
LAMINE YAMAL
Lamine Yamal mwenye umri wa miaka 16, katika mechi ya fainali atakuwa na miaka 17.
Amecheza mechi sita ambazo ametumia dakika 418, akifunga bao moja na kutoa asisti tatu, pia amejaribu kufanya mashambulizi mara 16 ikiwa ni wastani mara 2.67 kila mechi.
Amepiga kona nane, amekamatwa katika mtego wa kuotea mara mbili, amekokota mpira mara 30, pia kuingia katika boksi la adui mara 13.
Wastani wa kupiga pasi sahihi kwa asilimia 80.34 ambapo katika pasi 165 alizopiga kwenye Euro 2024, zilizofika ni 137.
Kati ya hizo, pasi fupi zilizokamilika ni 41 kati ya 53, pasi za umbali wa kati zilizowafikia wahusika ni 91 kati ya 103, vilevile pasi ndefu zilizofika ni sita kati ya 10.
Amepiga kasi za nyuma 53 zilizofika kati ya 56 za jumla, pasi za upande wa kushoto alizopiga 69 na zilizofika ni 52, zile alizopiga upande wa kulia ni 13 na zilizofika ni 11.
Katika upigaji wa krosi ana asilimia 38.47 za kupiga krosi zilizowafikia walengwa.
Lamine ambaye ameonyeshwa kadi ya njano moja, amefanya faulo saba na amefanyiwa faulo sita.
JUDE BELLINGHAM
Staa huyu wa England ambaye kwa sasa ana miaka 21, amecheza mechi sita ambazo ametumia dakika 481, amefunga mabao mawili, amerekodiwa kukimbia kwa spidi ya kilomita 33.5 kwa saa na amekimbia jumla ya kilomita 65.41.
Amepiga jumla ya pasi 326 na kati ya hizo zilizofika ni 288, kati ya hizo amepiga pasi fupi 90 na zilizofika ni 73, pia amepiga pasi ndefu 19 zikafika 16.
Vilevile amepiga pasi 70 za nyuma na zilizofika ni 67, alizopiga upande wa kushoto ni 67 na zilizofika ni 61, upande wa kulia zilizofika ni 104 kati ya 116 alizopiga.
Hayupo vizuri upande wa krosi kwani kati ya saba alizopiga hakuna hata moja iliyomfikia mlengwa, pia amecheza faulo tatu.
Katika mabao mawili aliyofunga, moja alitumia mguu wa kulia na moja akafunga kwa kichwa.
Jude amepata kadi za njano mbili katika faulo sita alizocheza, pia amechezwa vibaya mara 14.