Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuuzwa Man United, bodi inakutana

MANCHESTER, ENGLAND. KITU mashabiki wa Manchester United wanataka ni kusikia mchakato wa timu hiyo kuuzwa unakamilika.

Mashabiki wa Man United wamechoshwa na kuona sura za wamiliki wa klabu hiyo zikiendelea kubaki Old Trafford hivyo wanataka waje wawekezaji wapya wakiamini kuna mambo mengi yatabadilika.

Lakini, unakaribia mwaka sasa tangu Man United ilipotangazwa kuwekwa sokoni na matajiri wawili kati ya kadhaa waliojitokeza, wameonyesha dhamira ya dhati ya kuwa wamiliki wapya na wamekuwa wakichuana jino kwa jino kwenye zabuni zao za kuwa wamiliki wa miamba hiyo mabingwa wa kihistoria England.

Na sasa kinachoelezwa, Familia ya Glazer inayomiliki klabu hiyo kwa sasa, imepanga kufanya mkutano wa bodi ndani ya siku chache zijazo kujadili ofa mpya zilizowekwa mezani, hasa ya Bilionea Sir Jim Ratcliffe, kuona kama kuna biashara inaweza kufanyika na timu hiyo ikachukuliwa na bosi mpya.

Bilionea Mwingereza, Ratcliffe na hasimu wake mkuu kwenye vita ya kuinunua Man United, Sheikh Jassim bin Hamad Al Thani kila mmoja wameweka mezani ofa kadhaa za kutaka kuinunua timu hiyo tangu Familia ya Glazer ilipotangaza kuiweka sokoni Novemba 2022.

Tajiri Ratcliffe amekuja na mpango mpya wa kuwaambia Familia ya Glazer kwamba anataka kumiliki timu hiyo kwa hisa ndogo, asilimia 25 ili kuwashawishi wamiliki hao wa sasa kumpa nafasi ya kuingia kwenye bodi.

Mpango wa tajiri huyo wa Uingereza ni kuingia kwanza Man United, kisha aanze mchakato wa chinichini wa kununua hisa moja baada ya nyingine hadi hapo atakapokuwa mmiliki kamili baada ya mpango wa kuinunua jumla timu hiyo kwa kipindi hiki kuonekana kuwa mgumu kwa sababu kina Glazer hawataki kuachia timu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Bloomberg, familia nzima ya Glazer inajiandaa juu ya kuipiga bei jumla klabu hiyo ya Old Trafford ili kila mmoja aweke kibindoni mkwanja wake akafanye mambo yake.

Ofa ya kuinunua jumla Man United iliwekwa mezani na tajiri wa Qatari, Sheikh Jassim.

Mkutano mkuu wa bodi ya wakurugeni utakutana ndani ya siku chache zijazo, kujadili hatima ya timu hiyo, huku wamiliki wa sasa watapewa nafasi ya kuchakata maombi mapya kutoka kwa Ratcliffe kama yatakuwa na tija.

Bloomberg inaripoti kwamba hakuna uhakika kama Glazer watakubali ofa mpya ya Ratcliffe ya kutaka kumiliki hisa asilimia 25. Kinachoelezwa ni kwamba kuna uwezekano pia Sheikh Jassim akapandisha ofa yake kufikia kiwango kinachotakiwa na wamiliki hao wa Kimarekani ili naye atimize ndoto zake za kuimiliki Man United.

Tajiri wa Qatar, Sheikh Jassim anachotaka ni kuimiliki jumla Man United na si kuwa mwekezaji wa hisa chache.

Msimamo wake huo ambao ameweka mezani tangu alipoanza mchakato wa kuimiliki timu hiyo unaelezwa kuwa na nguvu zaidi kumzidi Ratcliffe, ambaye ameshindwa kuthibitisha ni kitu gani zaidi anataka baada ya kuibuka na ofa nyingine kutoka ile ya awali.

Mwanzoni Ratcliffe ofa yake iliyokuwa mezani ni kutaka kumiliki Man United kwa asilimia 65, huku akitoa nafasi kwa Familia ya Glazer kubaki kwenye timu hiyo. Lakini, kwa sasa amekuja na ofa ya kumiliki asilimia 25.

Sheikh Jassim anaitaka Man United kwa asilimia 100, huku akiahidi kuboresha miundombinu ikiwamo Uwanja wa Old Trafford, huku akiahidi kulipa madeni yote ya klabu hiyo na kuleta mastaa wa maana kikosini.

Wamiliki wa sasa wa Man United, klabu ambayo waliinunua tangu mwaka 2005, kwenye mchakato wa mauzo imeelezwa, wanafamilia wawili, Joel na Avram Glazer - ambao wapo mstari wa mbele kujihusisha na Man United, wanaripotiwa kutofautiana na ndugu zao linapokuja suala la kuuzwa timu hiyo.

Wanafamilia wengine wanataka timu hiyo iuzwe jumla ili kila mmoja achukue chake, wakati Joel na Avram bado wanang’ang’ania kubaki kwenye timu hiyo wakitaka kuuza nusu nusu, waendelee kubaki Old Trafford.

Kwa mujibu wa ripoti ya Sky iliyotolewa Oktoba, Familia ya Glazer inaithaminisha klabu yao kuwa na thamani ya Pauni 6 bilioni. Na ofa ya Ratcliffe ya asilimia 25 itamfanya amiliki baadhi ya hisa za Glazer na wanahisa wengine wadogowadogo waliopo kwenye klabu hiyo.

Bilionea huyo mmiliki wa Kampuni ya INEOS, Ratcliffe amekuwa na uzoefu wa kuhusu miliki klabu za michezo. Aliinua Klabu ya Lausanne-Sport ya Uswisi mwaka 2017 na miaka miwili baadaye aliichukua jumla Klabu ya Nice ya Ufaransa. Nice imekuwa ikimaliza nafasi za juu kwenye Ligue 1 katika kila msimu tangu ilipokuwa chini ya Ratcliffe. Msimu huu timu ipo kwenye nafasi ya pili. Kwa upande wa Lausanne, yenyewe imepanda daraja kurudi Ligi Kuu Uswisi msimu uliopita baada ya kushuka mwaka mmoja uliopita. Mambo yatakuwaje? Nani atashinda vita, Ratcliffe au Sheikh Jassim?