Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kuna Bocco wa Azam na wa Simba

Muktasari:

  • Mtu ambaye walisema amefikia mwisho wa maisha yake ya soka pale Chamazi. Mtu ambaye waliachana naye kwa mizengwe miezi michache nyuma. Mtu huyu ndiye amevaa kitambaa cha unahodha akiwaongoza wachezaji wenzake wa Simba katika mbio za ubingwa.

HEBU tafakari hii kidogo. Matajiri wa Azam wako mbele ya Luninga zao. Channel waliyoweka ni Azam Sports 2 wakitazama mechi ya Ligi Kuu Bara. Wanatazama mechi ya Simba ambayo staa wao wa zamani, John Bocco ni nahodha. Inakera sana.

Mtu ambaye walisema amefikia mwisho wa maisha yake ya soka pale Chamazi. Mtu ambaye waliachana naye kwa mizengwe miezi michache nyuma. Mtu huyu ndiye amevaa kitambaa cha unahodha akiwaongoza wachezaji wenzake wa Simba katika mbio za ubingwa.

Azam iliamini Bocco amekwisha lakini sasa ndiye anakaribia kuipa Simba ubingwa, akishirikiana vizuri na Emmanuel Okwi. Bocco anafunga karibu kila mechi. Asipofunga atatoa pasi ya bao. Yuko fiti kweli kweli.

Anawaongoza wachezaji wenzake kufanya vitu sahihi uwanjani. Uzuri, mastaa wote Simba wanamkubali Bocco. Ni nahodha mwenye heshima kubwa. Inaumiza sana kwa watu wa Azam sasa kumtazama Bocco.

Tayari amethibitisha hakuwa ameisha kama wao walivyotaka kutuaminisha. Mabao 14 aliyofunga Ligi Kuu mpaka sasa yamejibu maswali mengi yaliyokuwepo kwake. Kuna tofauti kubwa kati ya Bocco huyu wa Simba na yule wa Azam.

Bocco wa Simba amekuwa hatari zaidi. Ni mpambanaji zaidi. Ana kiu ya kufunga zaidi na anajituma zaidi ya alivyokuwa Azam. Nini kimetokea?

Kuna sababu kadhaa zilizomfanya Bocco wa sasa kuwa hatari zaidi. Kwanza kabisa ni timu anayocheza. Simba ina historia kubwa nchini. Simba inafuatiliwa na watu wengi zaidi na ina presha kubwa.

Ili ucheze kila siku pale Simba unatakiwa kujituma kweli kweli. Ukizubaa kidogo tu umeachwa. Hii imemfanya Bocco kucheza kila mechi kwa kiwango cha juu. Anafahamu kuwa akishuka kidogo tu benchi litamhusu.

Pale Azam Bocco alikuwa na uhakika wa kucheza kila siku.

Hata akifanya vibaya alikuwa akipangwa tena na tena. Makocha wa Azam walikuwa wakitafuta wachezaji 10 wa kucheza na Bocco kwenye kikosi cha kwanza. Alikuwa Mfalme kwenye nchi yake.

Sababu nyingine ya Bocco kucheza vizuri ni kutaka kuwatoa nishai wale waliokuwa wakibeza uwezo wake.

Kuna watu wanaoamini Bocco ni straika wa kawaida. Anachofanya Bocco kwa sasa ni kuwaonyesha hajawahi kuwa wa mchezaji wa kawaida. Mabao anayofunga yanaonyesha wazi kuwa ni mtu hatari.

Sababu ya tatu inayomfanya Bocco kuwa kwenye kiwango bora zaidi ni uwepo wa Emmanuel Okwi.

Pale Simba Okwi ndiye staa zaidi. Wanasimba wote wanamwamini Okwi, hawajawahi kuwa na mashaka naye.

Uwepo wa Okwi umemfanya Bocco kuwa mchezaji wa pili ama wa tatu muhimu ndani ya Simba. Okwi tayari alishathibitisha ni hatari ndani ya timu hiyo.

Amewahi kucheza Simba kwa mafanikio makubwa. Amewahi kushinda mataji mawili ya Ligi Kuu na Simba.

Uwepo wake umemfanya Bocco acheze kama mwendawazimu ili kuweka mambo sawa. Angalau amefanikiwa sasa na kila linapotajwa jina la Okwi ni lazima watu wamtaje na Bocco.

Pia kitendo cha Bocco kucheza pamoja na Okwi kimekuwa na faida kubwa kwao. Unapocheza na mtu anayejua vizuri soka, kazi yako pia inakuwa rahisi.

Utaona namna Okwi na Juma Liuzio walivyoshindwa kucheza pamoja kutokana na tofauti kubwa ya viwango vyao. Bocco na Okwi wanaenda vizuri.

Kwa Azam mambo yalikuwa tofauti. Baada ya kuondoka kwa Mrisho Ngassa kisha Kipre Tchetche, Bocco hakuwahi kucheza sambamba na mchezaji mwingine wa maana. Yeye ndio alikuwa staa zaidi.

Hebu kumbuka enzi zile, pale mbele kwenye kikosi cha Azam kuna Kipre na Bocco. Safu ya ushambuliaji ya Azam ilikuwa tishio. Kabla ya hapo kulikuwa na Ngassa, Kipre na Bocco. Ukicheza na Azam unaingiwa hofu.

Baada ya Ngassa kuondoka, kisha Kipre, Bocco alibaki peke yake. Aliletewa mastraika wa kawaida kama Allan Wanga, Yahya Mohammed na Samuel Afful. Azam yote ilimtegemea Bocco na hakukuwa na mbadala.

Akikosekana Bocco Azam yote inayumba. Bocco akikabwa vizuri Azam yote inayumba. Bocco hakuwa na mtu wa kumrahisishia kazi yake tena. Ni tofauti na pale Simba sasa, uwepo wa Okwi umemfanya acheze kwa ubora zaidi.

Hapa ndipo Azam ilipokuwa inakosea kwa Bocco. Kama timu yote inamtegemea Bocco kwa nini msione ameshuka kiwango? kila siku Bocco alitazamiwa kuibeba Azam, akiwa peke yake.

Mastraika wengine wote walishindwa. Msimu ukiisha unakuta Bocco ana mabao 10 halafu anayemfuatia ana matatu. Inachekesha sana.

Hebu tazama pale Yanga. Kulikuwa na Donald Ngoma na Amissi Tambwe. Kila mmoja alirahisisha kazi ya mwingine.

Ngoma alicheza zaidi, Tambwe akafunga zaidi. Mabeki wengi walipambana kumkaba Ngoma wakamsahau Tambwe.

Mnapokuwa wachezaji wawili wa viwango vya juu kazi yenu inakuwa nyepesi zaidi.

Tusione kama Bocco wa sasa ana miujiza sana, uhalisia ndio umemfanya awe kama alivyo. Angebaki Azam pengine angeendelea kuwa mchezaji wa kawaida.

Angeendelea kuwa mfalme na kucheza kawaida. Asingekuwa na msaidizi hivyo kusingekuwa na jipya sana.