Prime
Pacome, Ahoua utata wamalizwa

Muktasari:
- Kuna Jean Charles Ahoua, nyota wa zamani wa Stella Club d’Adjame, alikuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita 2023-2024.
VITA ya nani bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu imemalizika kibabe baada ya Yanga kuichapa Simba mabao 2-0, mjadala mkubwa uliobaki sasa Tuzo ya Mchezaji Bora (MVP) wa ligi hiyo itakwenda wapi ambapo vita hii imekuwa kali huku nyota wawili wakitajwa ambao wamewahi kubeba tuzo hiyo walipotoka.
Kuna Jean Charles Ahoua, nyota wa zamani wa Stella Club d’Adjame, alikuwa MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast msimu uliopita 2023-2024.
Mwingine ni Pacome Zouzoua ambaye pia alimaliza msimu wa 2022-2023 kwa kuibuka MVP wa Ligi Kuu ya Ivory Coast.
Wakali hao wanaocheza eneo la kiungo cha ushambuliaji, wote ni raia wa Ivory Coast na wanatajwa kuchuana vikali katika tuzo hiyo, hapa kuna mchango wa kila mmoja kuanzia kufunga, kutengeneza mabao na tuzo za mchezaji bora wa mechi.
MCHEZAJI BORA WA MECHI
Katika kila mchezo wa Ligi Kuu Bara ulipomalizika, amekuwa akichaguliwa mchezaji bora na Pacome amefanikiwa kuchaguliwa mara nane.
Kiungo huyo ndiye anaongoza kutwaa tuzo nyingi zaidi za mchezaji bora wa mchezo msimu huu akifuatiwa na Jean Charles Ahoua ambaye amechukua mara tano huku Yanga pia ikiwa kinara wa nyota wake kuchukua mara nyingi zaidi ikichukua mara 24 kati ya 30, Simba ikishika namba mbili kwa kuchukua mara 21 kati ya 30.
MCHEZAJI BORA WA MWEZI
Hapa Ahoua amechukua tuzo moja ya mchezaji bora wa mwezi na alifanya hivyo Agosti 2024, ikiwa ni mwanzo wa msimu huu.
Kwa upande wa Pacome, hajabeba tuzo hiyo ambayo mchezaji aliyechukua mara nyingi ni Steven Mukwala wa Simba akibeba mara mbili.
Orodha ya waliobeba tuzo hiyo kila mwezi ipo hivi; kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua (Agosti 2024), aliyekuwa mshambuliaji wa Fountain, Gate Seleman Mwalimu (Septemba 2024), kiungo wa Singida Black Stars, Marouf Tchakei (Oktoba 2024), kiungo wa Tabora United, Offen Chikola (Novemba 2024), mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize (Desemba 2024), mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube (Februari 2025), mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala (Machi 2025), kiungo wa Dodoma Jiji, Iddi Kipagwile (Aprili 2025) na mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala (Mei 2025).
TAJI LA LIGI
Pacome alijiunga na Yanga msimu wa 2023-2024 akitokea Ligi Kuu ya Ivory Coast alikokuwa mchezaji bora wa msimu (MVP) na alikuja kuongeza nguvu katika eneo la kiungo mshambuliaji akisaidiana na Stephane Aziz Ki, kinara wa upachikaji mabao msimu huo akifunga 21 ambaye ametimka hivi karibuni kwenda Wydad Casablanca ya Moroco.
Ahoua ameipambania Simba kusaka taji la ligi lakini imeshindikana, huku Pacome akihusika moja kwa moja kwenye mchezo wa uamuzi akifunga moja na asisti moja wakati Yanga ikishinda 2-0 dhidi ya Simba.
MCHANGO WA MABAO
Msimu huu, Ahoua ameibuka kinara wa mabao, kwa jumla amehusika kwenye mabao 25, akifunga 16 na asisti tisa. Pacome amefunga mabao 12 na asisti 10, hivyo amehusika kwenye mabao 22.
Huu ukiwa ni msimu wa kwanza kwa Ahoua, namba zake zimekuwa juu kulinganisha na ilivyokuwa kwa Pacome wakati anatua Yanga 2023-2024 na alipachika mabao saba na asisti nne akihusika kwenye mabao 11.
WASIKIE WENYEWE
Mara baada ya mechi dhidi ya Simba, Pacome alisema: “Kwa kweli ulikuwa msimu mgumu lakini mzuri. Tulipambana kama timu, tulijifunza kutoka kwa kila mchezo. Nafurahia kuchangia mafanikio ya Yanga. Tuzo binafsi ni zawadi ya juhudi, lakini kubwa ni kuona timu ikishinda taji. Kama nitachaguliwa kuwa MVP, nitashukuru sana.”
Ahoua naye hakusita kueleza hisia zake akisema: “Niliweka malengo makubwa nilipokuja Simba. Kufunga mabao 16 na kusaidia mengine tisa si jambo dogo. Tulitaka ubingwa lakini tumekosa kwa tofauti ndogo. Kuhusu MVP, kazi yangu ni kuichezea Simba kwa moyo. Kama nitashinda tuzo hiyo, nitakuwa na furaha sana kwa sababu inatoka kwa kile nilichoweka uwanjani.”
KAULI ZA WATAALAMU
Hivi karibuni, kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisema: “Pacome ni zaidi ya kiungo mshambuliaji, ni mtu anayejitolea kwa timu, anayeishi mchezo na kila mara hufanya maamuzi sahihi katika presha kubwa. Hawa ndio wachezaji unahitaji ili kushinda mataji.”
Kocha wa zamani wa Mtibwa Sugar na Gwambana, Mohammed Badru amemtaja Pacome kuwa ni MVP wake akisema: “Msimu huu MVP wangu ni Pacome. Wakati Ahoua alipofunga mabao matatu dhidi ya timu za katikati ya msimamo, Pacome alikuwa akiamua mechi kubwa kama dhidi ya Azam, Simba.”
Kwa upande wake, kocha wa zamani wa Simba Queens, Matty Mseti alisema: “Kwangu mimi Ahoua ndiye MVP. Bila yeye tungekuwa na msimu mbaya sana. Ni mfungaji mzuri, anakimbia, anajituma. Japokuwa Simba imepoteza ubingwa, Ahoua amekuwa na mchango mkubwa.”
HISTORIA YA MVP NA MWELEKEO WA MSHINDI
Katika miaka ya karibuni, MVP wa Ligi Kuu Bara amekuwa akitoka kwa timu bingwa. Hii inatoa picha, mafanikio ya timu hupewa uzito.
Tuzo hiyo msimu uliopita alishinda Stephane Aziz Ki alipokuwa Yanga, pia Clatous Chama alishinda msimu wa 2019-2020 wakati anaitumikia Simba na kubeba ubingwa wa ligi msimu huo.
Kwa misingi hiyo, Pacome ana nafasi kubwa hasa kutokana na ushindi wa Yanga na ushawishi wake mkubwa kwenye mechi za msimu huu.