Prime
Umemzingatia pilato Amin Omar?

Muktasari:
- Mchezo huo umeiingiza Tanzania kwenye historia mpya baada ya kuamuliwa na waamuzi kutoka Misri.
MCHEZO wa Dabi ya Kariakoo umemalizika ukihitimisha msimu wa Ligi Kuu Bara 2024-2025 na kutoa jibu la bingwa baada ya Yanga kuichapa Simba mabao 2-0, ushindi ambao umeifanya timu hiyo kutwaa ubingwa huo mara nne mfululizo na 31 kihistoria.
Mchezo huo umeiingiza Tanzania kwenye historia mpya baada ya kuamuliwa na waamuzi kutoka Misri.
Waamuzi hao walikuwa ni Amin Omar aliyesimama katikati, akisaidiwa na Mahmoud El Regal na Samir Mohamed huku mwamuzi wa akiba akiwa Ahmed Elghandour, hawa wote wakitoka Misri. Mtathimini waamuzi ni Ali Mohamed raia wa Somalia.

FILIMBI INASEMA, SIYO MDOMO
Dakika 90 za mchezo huo, Omar alionyesha uwezo mkubwa, akiiacha filimbi na akili yake kuamua matukio, huku akitumia mdomo wake mara chache sana kuzungumza pale ilipohitajika kama kumuonya mchezaji.
Mdomo wake ndani ya dakika 90 aliongea na wachezaji watatu pekee, akianza na Pacome Zouzoua pale alimpompa kadi ya njano kwa kosa la kujirusha kipindi cha kwanza, akaongea tena na Ellie Mpanzu kisha akamalizia na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alipokuwa analalamikia penalti ya mchezo huo. Wachezaji wengine wote walikaa naye mbali.
Filimbi zake hazikuwa nyingi sana kama ambavyo tumezoeshwa na waamuzi wetu wengi, alifanya hivyo pale alipohitajika kuipuliza na kuongeza ladha ya mchezo huo.

ANATEMBEA KWENYE MATUKIO
Omar alionyesha yuko sawasawa, alikuwa anafika kwenye maeneo inavyotakiwa, hakuamua kitu kwa umbali, alikuwa karibu na eneo linapotokea tukio na kuwafanya wachezaji wa timu zote kuridhika na kile alichoamua.
Sio tu kwa mwamuzi huyo wa kati, hata wasaidizi wake El Regal na Mohamed nao walikuwa na uamuzi sahihi kwenye kuzitega offside na wala hatukuona yale mambo ya mpira wa kutoka eti mwamuzi wa pembeni ndio anamuangalia mwamuzi wa kati aamue kipi.

AMEWAHESHIMISHA WALIOMTEUA
Hebu vuta picha waamuzi hawa wangekuwa na makosa kwenye mchezo huo na ukizingatia baada ya tu kutangazwa kwa majina yao klabu zote mbili zilionyesha kushtushwa zikidai hazikushirikishwa kwenye uamuzi huo.
Hapa waamuzi hawa wameliacha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kamati yake ya waamuzi kuwa salama kutokana na mshindi wa mchezo huo amepatikana kwa haki, hakukuwa na malalimiko.
TUNAO KINA OMAR
Ni suala la waamuzi wetu kuamua tu kulinda taaluma zao ambazo zitawauza sio tu ndani ya nchi hata kwenye mashindano ya Kiataifa.
Hapa nchini mwamuzi kama Omar yupo, mfano mzuri ni Ahmed Arajiga ambaye miaka ya karibuni amebadilika na kuwa mwamuzi anayesimama katikati kisawasawa na ndiyo maana sasa anakwenda sana kuchezesha mechi kubwa za Kimataifa.
Sio Arajiga tu hata waamuzi wa pembeni wapo kina Frank Komba, Kassim Mpanga na wengine ambao kama wataamua kutambua kutanguliza maamuzi yenye usahihi ni rahisi kwao kupata heshima kama hii ambayo kwa sasa inakwenda kwa Wamisri hawa.

YANGA, SIMBA WAMEFURAHI
Wakati waamuzi hawa wanatoka uwanjani baada ya mchezo, mashabiki wa Yanga na Simba wote wakajikuta wanawashangilia kwa kuridhika na maamuzi yao.
Huwa tunaona hata timu zinapokuwa zinakwenda mapumziko au mchezo kumalizika baadhi ya mashabiki wanaokaa pembeni ya eneo la timu kuingia vyumbani huwarushia maneno na hata chupa za maji, lakini haikuwa hivyo.
Hata majukwaani hakukuwa na malalamiko ya kwamba upande mmoja hauridhiki na kile kinachoamuliwa, kila kitu kilikwenda sawa kwa sheria za mchezo kuzingatiwa na hata timu iliyoshinda unasikia lawama zinakwenda kwa wachezaji na sio waamuzi.