Kumbe ishu ya Sesko ameumiza wengi
Muktasari:
- Sesko, 22, alikamilisha uhamisho wake wa kutua Old Trafford wiki iliyopita kwa dili la Pauni 74 milioni, ambapo italipwa Pauni 66.3 milioni kwanza na Pauni 7.4 milioni zitalipwa kama bonasi.
MANCHESTER, ENGLAND: KITENDO cha Manchester United kumnasa straika Benjamin Sesko hakikuacha tu masikitiko kwa Newcastle United bali kwa vigogo kibao Ulaya, imeelezwa.
Sesko, 22, alikamilisha uhamisho wake wa kutua Old Trafford wiki iliyopita kwa dili la Pauni 74 milioni, ambapo italipwa Pauni 66.3 milioni kwanza na Pauni 7.4 milioni zitalipwa kama bonasi.
Straika wa zamani wa RB Leipzig, Sesko aliweka kipaumbele chake kwenda kucheza Old Trafford licha ya kuwapo kwa timu nyingine kwenye Ligi Kuu England, Newcastle kuhitaji saini yake.
Hilo limetokea licha ya Man United kutokuwapo kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Hata hivyo, uhamisho huo wa Sesko kwenda Man United imeripotiwa kuiacha Barcelona kwenye maumivu makali, kwa mujibu wa gazeti la Sport.
Ripoti zinafichua miamba hiyo ya Camp Nou ilikuwa ikipiga hesabu za kwenda kumsajili Sesko na mkurugenzi wa michezo, Deco, alikuwa akikamilisha taratibu zake za mwisho ili akamnase staa huyo wa Slovenia.
Deco alimtazama Sesko kama mrithi sahihi wa straika Robert Lewandowski, 36.
Lewandowski amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na licha ya kwamba kuwapo na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja, lakini kinachoelezwa atafungasha virago vyake na kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Barca ilitambua kwamba Sesko yupo sokoni, lakini haikuwa na pesa za kutosha kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi ili kukamilisha dili la kumnasa.
Dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi lilishuhudia mastraika kadhaa wakihamia kwenye Ligi Kuu England, akiwamo Hugo Ekitike, aliyetua Liverpool na Viktor Gyokeres, aliyejiunga na Arsenal.
Barca ilidhani kwamba Sesko angeendelea kubaki Leipzig hadi mwakani ili ikamsajili, lakini Man United ikafanya kweli na hilo limewaumiza sana.