Mexico yaanza kumtisha Thomas Tuchel
Muktasari:
- Bao la mapema la Brian Cipenga katika dakika ya saba, liliipa DR Congo uongozi wa kushtukiza, lakini Harry Kane alifunga mabao mawili dakika 15 za mwisho za mchezo na kufikisha jumla ya mabao 13 ya Kombe la Dunia, akimpita gwiji wa Brazil, Pelé. Kati ya hayo, mabao matano ameyafunga katika mashindano ya mwaka huu.
ATLANTA, MAREKANI: WAKATI England ikifuzu hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia ambapo inakwenda kukabiliana na Mexico huko Mexico City, kocha mkuu wa kikosi hicho, Thomas Tuchel, amesema wanatarajia kukabiliana na vikwazo vingi vya ndani na nje ya uwanja ikiwemo hali ya mwinuko uliopo katika uwanja wanaochezea Jumapili hii.
England imefuzu hatua hiyo baada ya kutoka nyuma na kuifunga DR Congo mabao 2-1 mjini Atlanta, usiku wa kuamkia jana Alhamisi.
Bao la mapema la Brian Cipenga katika dakika ya saba, liliipa DR Congo uongozi wa kushtukiza, lakini Harry Kane alifunga mabao mawili dakika 15 za mwisho za mchezo na kufikisha jumla ya mabao 13 ya Kombe la Dunia, akimpita gwiji wa Brazil, Pelé. Kati ya hayo, mabao matano ameyafunga katika mashindano ya mwaka huu.
Mexico imecheza mechi tatu kati ya nne za Kombe la Dunia 2026 katika Uwanja wa Azteca, uliopo kwenye mwinuko wa takriban mita 2,240 (futi 7,220) juu ya usawa wa bahari. Wakati huo huo, England imeweka kambi yake Kansas City na hulazimika kusafiri kwenda kila eneo la mechi.
Taarifa zinasema kwamba, leo mchana England inatarajiwa kusafiri kwenda Mexico City kwa ajili ya kukabiliana na wenyeji wao ambao ni waandaji wenza wa michuano hiyo.
Akizungumzia mchezo huo, Tuchel amesema: “Nimetoka tu kumaliza mechi hii na ninajaribu kuifurahia, lakini huu ni miongoni mwa michezo mizuri na ya kusisimua zaidi unayoweza kuipata.
“Unacheza dhidi ya Mexico katika Uwanja wa Azteca, kutakuwa na vikwazo vingi sana vinavyotusubiri.
“Kuna suala la mwinuko ambao bila shaka utakuwa hasara kubwa kwetu kwa sababu hatuwezi kuuzoea kimwili ndani ya siku nne, lakini huenda kukawa na changamoto nyingine pia.
“Hata hivyo, tuko tayari kukabiliana nazo, labda tunahitaji changamoto kama hizi. Tumepata msingi mzuri wa kuamini kwamba tuko tayari, wakati mambo yatakapokuwa magumu, tutapata suluhisho.”
Awali, Ecuador iliwasilisha malalamiko rasmi kwa FIFA baada ya fataki kurushwa nje ya hoteli ya timu yao mjini Mexico City usiku uliotangulia kabla ya kufungwa 2-0 na Mexico.
Kuhusu hilo, Tuchel amesema: “Sina uhakika kama safari yetu itakwenda vizuri, kama tutapata usingizi mzuri au kama kutakuwa na kelele nje ya hoteli.
“Lakini hayo yote na yaje. Huu ni mchezo mzuri sana na wa kusisimua. Kutakuwa na changamoto nyingi, lakini timu hii itakuwa tayari kwa lolote litakalotokea.”
Hata hivyo, Tuchel alisisitiza kwamba England imekuwa ikijiandaa vizuri kwa hali ya hewa tangu ilipowasili Marekani kwa kambi ya maandalizi nchini Florida kabla ya mashindano kuanza.
Amesema: “Tulifika Marekani mapema sana na tukafanya mazoezi mengi katika hali ya joto ili miili ya wachezaji izoe hali hiyo. Hilo ndilo lilikuwa lengo letu.
“Ninaamini joto na unyevunyevu havitakuwa tatizo kwetu. Tumevizoea kupitia mazoezi na kipindi chetu cha maandalizi huko Florida.”
Lakini kuhusu mwinuko wa Mexico City, Tuchel amesema: “Kwa uelewa wangu, hatuwezi kuuzoea mwinuko huo. Hiyo ni faida kubwa sana kwa Mexico, kwa sababu kuzoea hali hiyo kunahitaji muda mrefu.
“Sisi tuna siku tatu tu kati ya mechi hii na inayofuata. Haiwezekani kabisa kuzoea mwinuko huo, ambao ni mkubwa sana.
“Tulijua hali hii mapema, hivyo ni hasara ambayo tutalazimika kuikabili. Lakini naamini tumeonyesha kwamba tuna mtazamo sahihi wa kupambana na changamoto hizo, hapo ndipo tutaanzia.”
Mshindi wa mchezo kati ya Mexico na England atakutana na mshindi wa mechi kati ya Brazil na Norway katika hatua ya robo fainali.