Kompyuta yatabiri Liverpool, Arsenal hazitoboi Top Four

LONDON, ENGLAND

MAMBO ni moto. Liverpool imetabiriwa kumaliza nje ya Top Four kwa mara ya kwanza tangu 2016, kwa mujibu wa Premier League Supercomputer.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England kwa sasa wapo kwenye nafasi ya sita baada ya kupoteza mechi nne mfululizo kwenye ligi, huku ikishuhudia mabao 10 yakitinga kwenye nyavu zao katika mechi hizo.

Jambo hilo, limekifanya kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp kuwa nyuma kwa pointi 19 dhidi ya vinara Manchester City na wamepitwa pointi tano na timu inayoshika nafasi ya nne kwa sasa, West Ham United.

Na kwa mujibu wa bettingexpert.com, miamba hiyo ya Anfield itacheza Europa League msimu ujao, kwa kuwa hawatashinda Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu na kwenye Ligi Kuu hawatakuwa kwenye nafasi nne za juu.

Wametabiriwa kwamba watamaliza msimu kwenye nafasi ya tano, huku Chelsea ikitabiriwa kukamilisha Top Four ya msimu huu kwenye mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England.

Chama la Pep Guardiola, Man City limeshinda mechi 19 mfululizo kwenye ligi hiyo na wametabiriwa kuwa ndio watakaobeba ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu huu.

Kama wataendelea na makali yao ya sasa, basi Man City itakwenda kushinda ubingwa wa tatu ndani ya misimu minne iliyopita.

Mahasimu wao Manchester United wametabiriwa watapiga hatua moja juu ya msimu uliopita kwa maana itamaliza msimu kwenye nafasi ya pili, huku Leicester City nayo ikitabiriwa kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwa maana ya kwamba itamaliza kwenye nafasi ya tatu msimu huu kwenye Ligi Kuu.

West Ham United waliopo kwenye nafasi ya nne kwa sasa, wametabiriwa watashuka kwa nafasi mbili na watashika namba sita mwisho wa msimu, huku Tottenham, Everton na Aston Villa zikimaliza chini yao.

Arsenal - ambayo imepoteza mechi tatu kati ya nne zilizopita kwenye ligi, wametabiriwa watamaliza msimu kwenye nafasi ya 10, ikiwa ni nafasi ya chini zaidi tangu msimu wa 1994-95, walipomaliza kwenye namba 12.

Leeds United inafanya vizuri kwenye msimu wake wa kwanza baada ya kurejea kwenye Ligi Kuu England na wanatabiriwa kumaliza ligi kwenye nafasi ya 11 kwa mujibu wa supercomputer.

Wametabiriwa kwamba watamaliza juu ya Wolves, Southampton, Crystal Palace, Brighton na Burnley.

Vichapo vitatu katika mechi nne za mwisho, Newcastle United waliopo kwenye nafasi ya 17 kwa sasa, kijasho kinawatoka kupambana kukwepa kurejea kwenye Championship.

Hata hivyo, supercomputer utabiri wake unaitoa hofu Newcastle United kwamba hawatamaliza ligi kwenye nafasi ya kushuka daraja, lakini shughuli ya kuporomoka ikiwahusu Fulham, West Brom na Sheffield United, kwamba supercomputer, inatabiri timu hizo zitacheza Championship msimu ujao.