Mourinho: Presha ni misha ya kila siku

Ushindi kidogo tu, Mourinho aanza kiburi

LONDON, ENGLAND 
KOCHA wa Tottenham Hotspur, Jose Mourinho ameonyesha kuizoea presha  kiasi cha kusema ni maisha yake ya kila siku hivyo wala hana hofu ya kuota nyasi kwa kibarua chake kufuatia mwenendo mbovu wa timu yake ambayo imekumbana na vipigo vitano kwenye michezo sita ya Ligi Kuu England.

Mourinho amesema  kwake  mara ya mwisho  kuwa na wakati mgumu  ilikuwa kipindi ambacho hakuwa na kazi  kwa karibu mwaka mzima,"Ni Shida ukiwa huna presha, kwangu presha ni kama hewa ya oksijeni, ni maisha yetu."

Akiongea kabla ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Burnley, kocha huyo wa zamani wa matajiri wa London, Chelsea na Manchester United ameongeza: "Sidhani kama  kuna kocha yeyote ulimwenguni ambaye hakumbani na presha."

Mwenendo mbovu wa Spurs katika michezo ya hivi karibuni  unaifanya timu hiyo kuwa nafasi ya  tisa wakiwa na pointi  36 huku wakiachwa kwa pointi tisa na West Ham ambao wapo katika nne bora lakini pia wameachwa kwa pointi 23 na vinara wa Ligi hiyo, Man City.

Spurs inaweza kufuzu msimu ujao kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya hata kama isipomaliza kwenye nne bora kwa sharti moja tu ambalo ni kutwaa ubingwa wa Europa Ligi ambayo wametinga hatua ya mtoano waliyopangwa kucheza dhidi ya  Dinamo Zagreb ya Croatia.

Akiongelea mashindano hayo, amesema,"Unapokuwa kwenye mashindano haya na kufikia hatua hii huwezi kupangwa na klabu nyepesi. Croatia ni  taifa la mpira, soka lao lipo juu na wamekuwa na wachezaji wenye vipaji, jambo muhimu kwetu ni kufika robo fainali."