KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Wanakwenda Qatar na watu wao kibao

DOHA, QATAR. UTAFITI umewataja masupastaa Cristiano Ronaldo, Lionel Messi na Neymar kuwamo kwenye orodha ya wanasoka 10 wenye kuhamasisha na mvuto mkubwa kwenye mtandao wa Instagram, ambao wanaotazamiwa kuwapo kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar.
Kipimo hicho kimefanywa kwa kuzingatia idadi ya wafuasi, kuongezeka kwa wafuasi, wastani wa wanaofuatilia kurasa za mastaa hao na thamani ya kila tozo inayotozwa kwa posti za matangazo zinazopostiwa na mastaa hao kwenye peji zao hizo za mtandaoni.
Na hilo limezingatiwa kwa wanasoka wanaopewa nafasi kubwa ya kuwapo na timu zao kwenye fainali za Kombe la Dunia 2022.
Utafiti huo umemtaja Ronaldo kuwa mtu mwenye mvuto zaidi kutokana na kuwa na ongezeko la wafuasi asilimia 48 ambao wameongezeka kwenye ukurasa wake kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Supastaa huyo wa Ureno ana wafuasi milioni 480 kwenye ukurasa wake huo wa Instagram, huku jambo hilo likimwingizia wastani wa Dola 3.6 milioni kwa kila posti ya tangazo la biashara analoweka kwenye peji yake.
Nafasi ya pili kwenye orodha hiyo, yupo mpinzani wake wa miaka yote kwenye soka, Messi. Mkali huyo wa Argentina amekuwa na wastani wa asilimia 38 ya ukuaji wa wafuasi wapya kwenye ukurasa wake walioongezeka kwa kipindi cha miezi 12 iliyopita, huku kila posti ya tangazo inayoonekana kwenye peji huyo, basi imetozwa mkwanja unaozidi Dola 2.7 milioni.
Staa anayeshikilia rekodi ya uhamisho duniani kwa sasa, Neymar - ambaye alinaswa na Paris Saint-Germain kwa mkwanja wa Pauni 198 milioni kutokea Barcelona mwaka 2017, anashika namba tatu kwa wanasoka wenye nguvu na mvuto mkubwa kwenye mtandao wa Ista ambao watakuwapo huko Qatar kwenye mchakamchaka wa fainali za Kombe la Dunia baadaye mwaka huu.
Neymar ana wafuasi milioni 178 kwenye ukurasa wake huo huku kila posti ya tangazo inayojitokeza kwenye ukurasa wake anachaji Dola 1.5 milioni. Staa mwenzake kwenye kikosi cha PSG, Messi anamiliki wafuasi milioni 360, huku pacha mwenzao kwenye fowadi ya matajiri hao wa Ufaransa, Kylian Mbappe ana wafuati milioni 72 na posti ya tangazo la biashara inayotokea kwenye ukurasa wake basi imemgharimu mwenye tangazo lake Dola 1.1 milioni.
Vinicius Junior anaibukia kwa kasi kwelikweli kutokana na kile anachofanya Real Madrid, ambacho kimemfanya kuvutia kwenye mtandao wa kijamii wa Insta. Vini Jr, wafuasi wake ni wachache ukilinganisha na Karim Benzema na Paolo Dybala, lakini kila posti ya tangazo inayotokea kwenye ukurasa wake inachajiwa pesa ndefu kuliko wakali hao, akichaji Dola 685,120 licha ya kuwa na wafuasi milioni 23, huku Benzema kwenye wafuasi milioni 58, kila posti ya tangazo anatoza Dola 489,239.
Wachezaji wengine ambao wanatazamiwa kuwapo Qatar 2022, ambao wanachipukia kwa kuwa na mvuto mkubwa kwenye mtandao wa Insta na pesa wanazotoza kwa kila posti za matangazo zinaoonyesha kwenye kurasa zao kwenye mabano.
Gavi (wafuasi milioni 6.2, Dola 377,305 kwa kila posti), Raphinha (milioni 3, Dola 22,727), Anthony (milioni 4.8, Dola 106,229), Pedri (milioni 7.3, Dola 255,212), Rodrigo de Paul (milioni 5, Dola 206,983), Rodrygo Goes (milioni 7.5, Dola 119,726), Aurelien Tchouameni (milioni 2.1, Dola 80,973), Achraf Hakimi (milioni 10.1, Dola 133,187), Dusan Vlahovic (milioni 1.7, Dola 118,691) na Darwin Nunez wafuasi milioni 2.1 na kila posti anatoza Dola 14,527.
Mastaa wengi kwenye orodha hii wanaochipukia kama Nunez, thamani wanazotoza kwa kila posti za matangazo zinazotokea kwenye kurasa zao za Insta zimeongezeka baada ya kujiunga na klabu kubwa za Ulaya, ambapo mkali huyo alitua Liverpool kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kwa mkwanja wa Pauni 85 milioni.