KOMBE LA DUNIA QATAR 2022: Tielemans atakavyo kwenda kujiuza Qatar 2022

Summary


Doha, qatar. STAA wa Leicester City, Youri Tielemans, 25, ambaye katika dirisha lililopita la uhamisho alihitajika na Arsenal, ana nafasi kubwa ya kutua kwenye kikosi hicho katika dirisha lijalo baada ya fainali za Kombe la Dunia.

Mkataba wake utamalizika mwisho wa msimu huu na amegoma kusaini mkataba mpya, hivyo katika kujihami Leicester inaweza kumuuza Januari.


Rafael Leao

STAA wa AC Milan na Ureno, Rafael Leao, 23, ni miongoni pia mwa wachezaji wenye nafasi kubwa ya kusajiliwa na timu nyingine katika dirisha la Januari baada ya fainali za Kombe la Dunia kwani amekuwa akiwindwa na timu nyingi ikiwemo Chelsea. Mabosi wa Chelsea walitamani kumpata staa huyu dirisha la majira ya kiangazi lakini ilishindikana kutokana na kiasi cha pesa ilichoweka.


Ruben Nevez

Vigogo wa Barcelona wameanza kuwasiliana na wawakilishi wa kiungo wa Wolves na Ureno, Ruben Nevez, 25, ili kumsajili katika dirisha lijalo akawe mbadala wa Mhispania Sergio Busquets, 34, ambaye kuna uwezekano akaondoka mwisho wa msimu huu.

Dili hilo linatarajiwa kukamilika mara baada ya staa huyo kutoka kwenye michuano ya Kombe la Dunia akiwa na Timu ya Taifa ya Ureno.


Jude

Bellingham

Ikiw ataonyesha kiwango bora kuna uwezekano vigogo wa soka Real Madrid, Chelsea, Liverpool na Manchester United wakawasilisha ofa kwa Borussia Dortmund ili kuipata huduma ya kiungo wa timu hiyo na England, Jude Bellingham, 19, katika dirisha lijalo.

Bellingham amekuwa akiwindwa na timu nyingi barani Ulaya tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini Dortmund iligoma kumuuza.


Lionel Messi

Mazungumzo baina ya mabosi wa Paris St-Germain na wawakilishi wa staa wao Lionel Messi, 35, yamesitishwa kwa sasa hadi Kombe la Dunia itakapomalizika.

Mazungumzo hayo yalisimama baada ya Messi mwenyewe kudai hatatoa jibu lolote la kueleweka hadi atakapocheza michuano hiyo.

Taarifa za ndani zinadai staa huyo hana mpango wa kuendelea kusalia kwenye kikosi hicho kwani anahitaji kutimkia Marekani.


Cristiano Ronaldo

Baada ya kumalizika kwa Kombe la Dunia, mabosi wa Man United watakaa chini na wawakilishi wa Cristiano Ronaldo kujadili hatma yake ambapo inadaiwa kuna uwezekano akaondoka katika dirisha lijalo la majira ya baridi.

Ronaldo alihitaji kuondoka tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini mabosi wa Man United hawakuonekana kuwa tayari kumuachia licha ya ofa nono zilizowasilishwa mezani kwao kutoka timu za Uarabuni na Ulaya.


Memphis Depay

Barcelona inafikiria kumuuza, Memphis Depay, 28, dirisha lijalo la majira ya baridi baada ya Kombe la Dunia. Ilijaribu kumuuuza katika dirisha lililopita lakini mambo yalikuwa magumu kwani timu nyingi zilikataa kutoa pesa zikiamini jamaa kiwango chake kimeshuka.


Federico Valverde

Baada ya kuikosa saini yake dakika za mwisho za dirisha la kiangazi, Liverpool imeripotiwa kutakakuwasilisha ofa Real Madrid ili kuipata saini ya kiungo wa timu hiyo na Uruguay, Federico Valverde, 24.

Valverde ni tegemeo katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Uruguay ambacho kitashiriki Kombe la Dunia. Liverpool inahitaji kiungo na mmoja kati ya wale wanaopewa kipaumbe kuelekea dirisha lijalo la usajili la majira ya baridi Januari 2023 ni fundi huyu wa Madrid.