Kocha Simba ainyima taji Nigeria
Muktasari:
- Super Eagles imefuzu hatua ya 16 Bora ikiwa na rekodi kamili baada ya kukusanya pointi tisa katika mechi tatu katika kundi lililokuwa na nchi za Tanzania, Uganda na Tunisia.
KOCHA wa zamani wa Simba, Dylan Kerr aliyewahi pia kuzinoa Gor Mahia ya Kenya na Moroka Swallows ya Afrika Kusini, ameshindwa kujizuia na kutoa sababu zinazomfanya aamini kuwa Nigeria na Afrika Kusini zina nafasi ndogo ya kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 linlofanyika Morocco.
Super Eagles imefuzu hatua ya 16 Bora ikiwa na rekodi kamili baada ya kukusanya pointi tisa katika mechi tatu katika kundi lililokuwa na nchi za Tanzania, Uganda na Tunisia.
Chini ya kocha raia wa Mali, Eric Chelle, Super Eagles ilianza kampeni ya Kundi C kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania, kisha mechi ya pili dhidi ya Tunisia ilishinda 3-2 na kumalizia kwa kufumua Uganda mabao 3-1, ikiwa ni moja ya timu mbili pekee zilizoshinda mechi za makundi kwa asilimia 100 sambamba na Algeria.
Nigeria kesho inatarajiwa kukutana na Msumbiji katika mechi hiyo ya mtoano ambapo Mambas ilifika hatua hiyo baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Gabon na kuifanya ihitimishe miaka 40 ya kusubiri ushindi wa kwanza katika AFCON, ikimaliza nafasi ya tatu ya Kundi F ikiwa na pointi tatu na kufuzu 16 Bora kwa mara ya kwanza kabisa.
Licha ya kuwa na kikosi chenye wachezaji nyota kama Victor Osimhen, Ademola Lookman na Alex Iwobi, miongoni mwa wengine, kocha Kerr, raia wa Uingereza ambaye kazi yake ya mwisho ya ukocha ilikuwa na Marumo Gallants ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini, hana imani kama Nigeria ina kila kitu kinachohitajika kutwaa ubingwa.
“Nigeria inapaswa kuwa na timu nzuri, lakini haikufuzu moja kwa moja Kombe la Dunia, kwa hiyo kuna kitu hakiko sawa katika mchezo wao,” Kerr mwenye umri wa miaka 58 aliiambia Flashscore katika mahojiano ya maalumu.
Super Eagles ilikosa tiketi ya Kombe la Dunia la FIFA 2026 baada ya kufungwa kwa penalti 4-3 na DR Congo katika mechi ya mwisho ya mchujo wa Afrika huko Morocco. Hii ilikuwa mara ya pili mfululizo kukosa ushiriki wa Kombe la Dunia kwani ilizokosa pia zile za 2022.
Alipoulizwa kwa nini Nigeria, licha ya kuwa na rekodi ya asilimia 100 katika makundi, haiwezi kushinda AFCON, Kerr amesema:
“Si rahisi. Ushindi wote katika hatua ya makundi unaweka presha kubwa kwao. Mara nyingi, timu zinazopata shida mwanzoni ndizo huishia kufika nusu fainali au fainali.”
Kuhusu iwapo Nigeria itavuka dhidi ya Msumbiji, amesema: “Huwezi kujua. Itakuwa mechi ngumu na inaweza kwenda upande wowote. Naiona Msumbiji ikiipa Nigeria upinzani mkali.”
Akiulizwa ni nani anaona atatwaa ubingwa wa AFCON 2025, Kerr amesema: “Ni vigumu kusema. Cameroon itakuwa kibarua kigumu kwa Afrika Kusini.
“Msumbiji wamefanya vizuri. Misri na Morocco wamefuzu kwa urahisi, Sudan imenishangaza, Tunisia imekutana na mechi ngumu dhidi ya Mali na Morocco inapaswa kuifunga Tanzania.”
Tunisia imetolewa kwa penalti 3-2 na Mali, wakati Tanzania na Morocco zilikuwa uwanjani usiku wa jana.
Kuhusu Afrika Kusini kukutana na Cameroon, amesema: ”Afrika Kusini haijacheza vizuri katika mechi zao tatu za mwisho, kwa hiyo mechi hiyo itakuwa ya kuvutia.€
“Algeria dhidi ya DR Congo itakuwa mechi nzuri, na nina hisia kuwa Ivory Coast watashinda mechi yao. Ivory Coast wana kikosi imara, lakini kwa maoni yangu, Morocco ndiyo inaongoza kwa nafasi ya kushinda AFCON kwa kuwa ni wenyeji.”
Kerr aliongeza kwa kusema; “Hatua za mtoano huwa za kuvutia sana. Hapa ndipo mechi zinakuwa ngumu zaidi; timu hazitaki kupoteza kwa sababu kupoteza kunamaanisha safari imeisha.
“Kila mtu anakuwa mwangalifu kushambulia, au anajaribu kufunga bao moja kisha kulilinda. Katika hatua hii, kila kitu huhesabika.”
Nigeria itacheza na Msumbiji kesho kwenye Uwanja wa Fez, huku ikiwa na rekodi ya kutwaa taji hilo mara tatu ikifanya hivyo 1980 ikiwa wenyeji, 1994 pale Tunisia na 2013michuano hiyo ilipofanyikia Afrika Kusini.