Kocha mpya Chelsea ataka njia za Ferguson
Muktasari:
- Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi habari, Rosenior amesema yeye anaitazama Chelsea kama vile Man United ya “Class of ’92” ambayo ilipata mafanikio makubwa ikiwa na wachezaji wenye umri mdogo.
LONDON, ENGLAND: KOCHA mpya wa Chelsea, Liam Rosenior amesema ni mkubwa sana licha ya baadhi ya watu kubeza kwamba timu ina watoto wengi.
Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi habari, Rosenior amesema yeye anaitazama Chelsea kama vile Man United ya “Class of ’92” ambayo ilipata mafanikio makubwa ikiwa na wachezaji wenye umri mdogo.
Rosenior amesema kuwa yeye ndiye atakayefanya maamuzi yote katika klabu hiyo licha ya kuwepo kwa ripoti kwamba uongozi wa juu ndani ya Stamford Bridge ndio unalodhibiti kila kitu.
Kocha huyo mwenye urai wa England na Seira Leone pia aliomba mashabiki wa Chelsea wampe imani ili aweze kuifikisha timu katika nchi ya ahadi.
Alipoulizwa kama anaweza kubadilisha timu ya vijana zaidi katika historia ya Ligi Kuu kuwa washindi wa mataji msimu huu au ujao, Rosenior mwenye umr wa miaka 41, amesema: "Niliulizwa swali sawa na hili miezi 18 iliyopita nilipojiunga na Strasbourg. Hakuna kitu kizuri zaidi kuliko kuwa kwenye safari na kikundi cha wachezaji wenye umri mdogo.Nakumbuka Sir Alex Ferguson alikuwa jasiri vya kutosha kuingiza wachezaji sita au saba wenye umri wa kati ya miaka 19 na 21 katika timu yake, na timu hiyo ikashinda mataji, unajua kwanini? ni kwa sababu aliwaamini."
"Walikomaa na kushinda taji baada ya taji. Kipindi hicho kilikuwa cha kipekee katika historia ya klabu yao. Bila ujasiri huo wa Ferguson, hilo lisingewezekana."
a'Kuna uwezekano wa kufanya vivyo hapa pia. Uwezekano upo lakini sio kwa sasa. Watazame Moises Caicedo, Enzo Fernandez, Cole Palmer au Reece James ni wachezaji wa kiwango cha dunia na bado vijana sana. Hii ndiyo ndoto ya klabu hii, kuwa na wachezaji wakubwa wenye umri mdogo."
“Sijajaribu kusema kwamba nitaifikia hiyo ndoto na itatimia. Nimeonyesha nikiwa na Strasbourg kwamba naweza kufanya kazi na wachezaji vijana, kuwaweka vizuri na kushinda mechi hivyo hakuna sababu ya kushindwa kufanya nikiwa hapa."
Akizungumzia watu wanaosema kwamba hana sifa za kuwa kocha wa Chelsea kwa sababu CV yake sio kubwa, Rosenior amesema:"Kila mtu huanza mahali fulani. Kuna nukuu nzuri kutoka kwa Mourinho, ambaye ni shujaa wangu. Nimejifunza kutoka kwake. Amesema ilimchukua “miaka 20 kuwa na mafanikio kwa mara ya kwanza.” Ndivyo ilivyo kwa kila mtu."
“Hukumu yako iwe kwa kile unachokiona. Usihukumu kwa kile unachosikia. Usihukumu mikutano yangu na waandishi wa habari. Siwezi kushinda mechi nikiwa mkutanoni nihukumu kwa kile unachokiona uwanjani. Nipe mimi, wafanyakazi wangu na wachezaji wangu nafasi ya kuthibitisha kuwa tunastahili badala ya kunikataa kabla sijaanza hiyo kazi yenyewe. Tuhukumu kwa haki, mimi mwenyewe nikiona sitoshi nitakuwa wakwanza kunyanyua mikono juu."