Kiroho safi, Maresca aacha mabilioni Chelsea
Muktasari:
- Muitaliano huyo, mwenye umri wa miaka 45, aliondoka katika viunga vya Stamford Bridge siku ya Mwaka Mpya baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni kuvunjika kwa uhusiano wake na bodi ya klabu hiyo.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Chelsea, Enzo Maresca anadaiwa kuwa amekataa malipo ya mamilioni ya Pauni baada ya kuondoka Chelsea.
Muitaliano huyo, mwenye umri wa miaka 45, aliondoka katika viunga vya Stamford Bridge siku ya Mwaka Mpya baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni kuvunjika kwa uhusiano wake na bodi ya klabu hiyo.
Licha ya mgongano huo mkali uliomfanya ashindwe kuendelea, tovuti ya The Sun imefichua kwamba kocha huyu amekataa kulipwa fidia ya takribani Pauni 14 milioni (Sh46 bilioni).
Alipojiunga na Chelsea akitokea Leicester mwaka 2024, Maresca alisaini mkataba wa miaka mitano ukiwa na chaguo la mwaka mmoja zaidi ambao ulikuwa unamwezesha kukunja mshahara wa takriban Pauni 4 milioni kwa msimu.
Siku ambayo anafungashiwa virago baada ya kuhudumia kwa miezi 18 tu, alitakiwa kulipwa fidia ya mshahara ya Pauni 14 milioni ambao alitakiwa alipwe endapo angekaa hadi mwisho wa mkataba wake.
Kuondoka kwa Maresca kulitokea chini ya miezi mitano baada ya kushinda taji la Kombe la Dunia la FIFA na Uefa Conference League akiwa na matajiri hao.
Inaelezwa Maresca alikuwa na hasira sana kwa sababu aliona anakandamizwa na mabosi wa Stamford Bridge na hiyo ilimfanya aondoke bila ya kufanya majadiliano kuhusu stahiki zake.
Vyanzo vya ndani vya Chelsea vimemlaumu kocha huyu kwa kukosa ukomavu wa kiakili, pia vimempa shutuma ya alijaribu kutumia ofa kutoka Juventus na Manchester City ili kuilazimisha Chelsea kumpa mkataba mpya, lakini hili limekanushwa vikali na wawakilishi wake.
Taarifa za ndani zinadai pia mabosi wa Chelsea walikuwa na hasira juu ya Maresca kutokana na kile kinachoelezwa kwamba hakuwa akiangalia maslahi na afya za wachezaji na aliwahi kuwatumia mastaa kama Reece James na Cole Palmer wakati timu ya madaktari ilishashauri kuwa wasitumike.
Hata hivyo, haya yalikuwa yanaonekana tofauti kwa Maresca ambaye alikuwa akichukizwa sana na hali hiyo kwani aliamini yeye ndio mfalme wa jambo lolote la uwanjani na hakutakiwa kuingiliwa kwa namna yoyote.
Inaelezwa pia kuna nyakati viongozi walikuwa wakimpigia simu au kumwambia ana kwa ana kwamba nani anatakiwa kuanza na nani asianze jambo ambalo halikumpendeza pia kocha huyu.
Maresca aliachana na Chelsea baada ya sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya Bournemouth Jumanne.