Kocha Crystal Palace awachana matajiri
Muktasari:
- Glasner alitema nyongo baada ya Palace kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sunderland katika Ligi Kuu England wikiendi iliyopita.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Crystal Palace, Oliver Glasner amesema viongozi wa timu hiyo wamewatelekeza yeye pamoja na wachezaji hali inayoendelea kuzorotesha kiwango cha timu kila siku.
Glasner alitema nyongo baada ya Palace kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Sunderland katika Ligi Kuu England wikiendi iliyopita.
Palace ilikuwa mbele kwa bao 1-0 la Yeremy Pino kwenye Uwanja wa Stadium of Light, lakini mabao ya Enzo Le Fee na Brian Bobbey yaliilazimisha timu hiyo kukubali kipigo, siku moja tu baada ya Glasner kutangaza ataondoka klabuni hapo mwisho wa msimu.
Kocha huyo raia wa Austria aliiongoza Palace kutwaa taji lao la kwanza kubwa Mei mwaka jana walipoifunga Manchester City Wembley na kushinda Kombe la FA, kabla ya kuifunga Liverpool kwa mikwaju ya penalti katika mechi ya ngao ya hisani.
Hivi karibuni alikuwa akihusishwa na timu kadhaa kabla ya kusema wazi anataka kuondoka na kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Baada ya mechi dhidi ya Sunderland, Glasner aliweka wazi hasira zake kuhusu kuondoka kwa Eberechi Eze na Marc Guehi, hususan mazingira ya namna walivyouzwa kwani wote waliuzwa siku moja kabla ya Palace kucheza mechi.
Nahodha Guehi alionekana karibu kujiunga na Liverpool siku ya mwisho ya dirisha la usajili wa majira ya joto kabla ya dili hilo kuvunjika dakika za mwisho. Baadhi ya taarifa zilidai Glasner alitishia kuondoka endapo Guehi angeuzwa.
Hata hivyo, beki huyo wa England anatarajiwa kuondoka dirisha hili la Januari na kujiunga na Manchester City kwa dau la Pauni 20 milioni, miezi michache tu kabla ya mkataba wake na Palace kumalizika.
“Ninahisi kama tumetelekezwa kabisa,” Glasner aliambia BBC.
“Siwezi kumlaumu mchezaji yeyote, walifanya kila walichoweza. Tuna wachezaji 12 au 13 tu waliopo tayari kuanza kwenye kikosi. Jambo baya zaidi ni kumuuza nahodha wetu siku moja kabla ya mechi ya Ligi Kuu. Sikushirikishwa juu ya hili."
"Nimekuwa nikinyamaza lakini sasa siwezi, kwa sababu lazima niwatetee hawa wachezaji. Moyo wako ukivunjwa mara mbili katika msimu mmoja na kila mara siku moja kabla ya mechi hiyo haikubaliki, ilitokea kwa Eberechi Eze na sasa kwa Marc Guehi. Nitawaambia nini wachezaji juu ya hiki kinachoendelea?"
Licha ya kutoridhishwa sana na hali hiyo, Glasner alisisitiza hataondoka na kuwaacha wachezaji wake katika kipindi hiki kigumu.
“Hapana, kamwe, sitafanya hivyo,” amesema.
“Nitaendelea kuwa na kundi hili la wachezaji hadi mwisho.
“Ninaheshimu sana juu walivyo na tabia nzuri. Naona wamevunjika moyo lakini najua wanajituma kwa bidii, naona jinsi wanavyopambana hadi mwisho. Kamwe, haiwezekani mimi kuwaacha kwa sasa."