Marc Guehi mlango wazi kusepa
Muktasari:
- Kocha wa Palace, Oliver Glasner, mapema wiki hii alithibitisha kwamba beki huyo anaweza kuuzwa baada ya kuzuia dili lake la kuondoka mwaka jana.
MANCHESTER, ENGLAND: BEKI wa Crystal Palace, Marc Guehi anaweza kuondoka Crystal Palace mwezi huu ikiwa Manchester City itakubali kutoa Pauni 40 milioni ambayo ni ada yake.
Kocha wa Palace, Oliver Glasner, mapema wiki hii alithibitisha kwamba beki huyo anaweza kuuzwa baada ya kuzuia dili lake la kuondoka mwaka jana.
Man City inaonekana kutamani sana huduma ya fundi huyu kutokana na msururu wa majeruhi katika safu yao ya ulinzi.
Ruben Dias na Josko Gvardiol watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha waliyoyapata hivyo itailazimu timu hiyo kupata mbadala wao mapema iwezekanavyo.
Hata hivyo, mbali ya ada ya uhamisho ambayo Palace inahitaji, Man City itatakiwa kumpa ofa nono ya bonasi ya usajili fundi huyu ambaye akisubiri hadi mwisho wa msimu na kuondoka akiwa huru anaweza kukunja pesa nyingi sana kama bonasi yake ya usajili.
Akizungumzia kuondoka kwa staa huyo, kocha Glasner amesema: “Itafikia wakati ambapo klabu itasema sasa suala la fedha ni muhimu zaidi. Mimi si mjinga kiasi cha kutojua kwamba ikitokea ofa kubwa kutoka Man City na Marc akataka kuondoka, klabu itamzuia, hapana. Najua tu ataondoka.”
Palace ilisitisha mpango wa kumuuza staa huyu kwa Pauni 35 milioni kwenda Liverpool siku ya mwisho ya dirisha la usajili la majira ya kiangazi mwaka jana, na sasa imeongeza bei kwa sababu italazimika kutafuta mbadala wake mwezi huu ikiwa itamuuza.
Glasner alikuwa tayari anatafuta mabeki wapya na alifichua kuwa, kabla ya mabeki wawili wa Man City kupata majeraha makubwa, walikuwa wanaangalia uwezekano wa kumsajili mmoja wa mabeki wa kikosi hicho.
“Tulitaka kununua mchezaji kutoka Man City na sasa hatuwezi tena, kwa sababu wao pia wana majeruhi.”