Kocha Arsenal alia na ratiba EPL
Muktasari:
- Kiungo wa washika mitutu hao, Declan Rice aliondoka uwanjani akichechemea kutokana na jeraha la kiazi cha mguu (kigimbi) wakati Arsenal ikiifunga Brentford mabao 2-0 na ikiendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta amekosoa ratiba ya Ligi Kuu England akidai inachangia sana katika majeraha ya wachezaji wa klabu ikiwamo Arsenal.
Kiungo wa washika mitutu hao, Declan Rice aliondoka uwanjani akichechemea kutokana na jeraha la kiazi cha mguu (kigimbi) wakati Arsenal ikiifunga Brentford mabao 2-0 na ikiendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi tano.
Mikel Merino na Bukayo Saka ndio walifunga mabao yaliyoiwezesha Arsenal kufikisha mechi 18 bila kupoteza na kuendelea kuongoza ligi.
Hata hivyo, ushindi huo ulikuja na gharama yake baada ya Rice na Cristhian Mosquera kulazimika kutoka nje baada ya kuumia.
Mastaa hao sasa wanaongeza idadi ya wachezaji majeruhi wa Arsenal katika kipindi hiki ambacho timu hiyo inapambania taji la EPL.
Mosquera alianza pamoja na Piero Hincapie kutokana na kutokuwapo kwa William Saliba na Gabriel Magalhaes ambao wanauguza majeraha.
Arteta ambaye anaamini mechi zimekuwa mfululizo kiasi cha kukosa mapumziko, kikosi chake kilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa katikati ya wiki iliyopita dhidi ya Bayern Munich kikitokea kucheza London Derby dhidi ya Tottenham kabla ya kuivaa Chelsea Jumapili na juzi kucheza dhidi ya Brentford.
Hata hivyo, baada ya kucheza na Brentford, Jumatano, kesho itakuwa tena dimbani kuvaana na Aston Villa katika mwendelezo wa EPL.
Saliba, Gabriel, Kai Havertz na Leandro Trossard wote wanauguza majeraha wakati Martin Odegaard, Noni Madueke na Viktor Gyokeres wakiwa ndio wamerejea hivi karibuni baada ya kukosekana kwa muda kutokana na majeraha pia.
"Si habari njema, Declan alilazimika kutoka nje. Hatujui bado ameumia kiasi gani, tutalazimika kusubiri kesho tuone ukubwa wa tatizo baada ya kufanyiwa vipimo zaidi.
"Hakuweza kuendelea kucheza. Anaweza kutembea. Amecheza dakika nyingi sana, lakini pia angalia ratiba ilivyo, tumecheza leo Jumatano usiku kisha tena Jumamosi asubuhi.
"Naomba kama tunaweza kuongezewa muda wa kupumzika, itakuwa bora kwa ustawi wa wachezaji, tunaomba walau siku moja zaidi hasa kwa timu zinazoshiriki michuano ya Ulaya. Wachezaji sio mashine."