Gyokeres akusanya kijiji chake
Muktasari:
- Na hilo ni rahisi kulielewa kwanini. Gyokeres anajitolea sana, anapambana sana na anafanya kila anachoweza ndani ya uwanja. Na hilo ndilo linalomfanya awe kipenzi cha mashabiki wa miamba hiyo ya Emirates na kuwa maarufu kuzidi Kai Havertz, Gabriel Jesus na hata Mikel Merino.
LIVERPOOL, ENGLAND: STRAIKA, Viktor Gyokeres ameteka mioyo na akili za mashabiki wa Arsenal.
Na hilo ni rahisi kulielewa kwanini. Gyokeres anajitolea sana, anapambana sana na anafanya kila anachoweza ndani ya uwanja. Na hilo ndilo linalomfanya awe kipenzi cha mashabiki wa miamba hiyo ya Emirates na kuwa maarufu kuzidi Kai Havertz, Gabriel Jesus na hata Mikel Merino.
Gyokeres alisajiliwa kwa Pauni 64 milioni na kuwa Namba 9 wa Arsenal na alitoka kufunga mabao ya kutosha sana kwa miaka yake miwili alipokuwa Sporting Lisbon. Sawa kwa sasa bado hajawasha ule moto kwenye kufunga mabao tangu alipotua Arsenal kutokana na kutikisa nyavu mara sita tu tangu alipojiunga na wababe hao wa London Kaskazini.
Lakini, Gyokeres amekuwa maarufu kwa mashabiki wa Arsenal kwa sababu amekuwa ni straika wa kizamani, ana nguvu na anapambana kwa kila vita ndani ya uwanja. Ni mpambanaji. Mashabiki wanaimba nyimbo za kulitaja jina lake kutokana na kile anachokifanya ndani ya uwanja.
Anapiga kazi, anawakaba na kuwapa wakati mgumu mabeki wa timu pinzani. Ukweli, Gyokeres anaipa Arsenal kitu tofauti. Na anapenda kuzengeazengea kwenye goli la timu pinzani na kuwa ndani ya boksi muda wote kutafuta nafasi ya kuusukumia mpira nyavuni.
Gyokeres alikuwa nje ya uwanja kwa wiki kadhaa kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli, lakini alirejea uwanjani dhidi ya Chelsea na kuonyesha kiwango cha ubora wa hali ya juu. Upambanaji wake ulimfanya aburuzike kuwahi mpira uliokuwa umezagaa na hivyo kungongana na kipa wa Chelsea, Robert Sanchez. Gyokeres yupo tayari kufanya chochote ndani ya uwanja kwa ajili ya timu yake hata kama ataonyeshwa kadi ya njano. Ana njaa.
Mashabiki wa Arsenal wanaamini suala la kufunga mabao kwa Gyokeres ni la muda tu, litakuja na sasa kinachosubiriwa ni wachezaji wenzake kuanza kumpa pasi muhimu kwenye maeneo muhimu.
Usiku wa Jumatano wakati Arsenal ilipokuwa na mechi dhidi ya Brentford iliaminika Gyokeres angeendeleza makali yake ndani ya uwanja na kuwapa wakati mgumu mabeki wa timu pinzani.
Ujio wake kwenye kikosi cha Arsenal unaleta mtihani mkubwa kwa Havertz, ambaye ni kipenzi cha kocha Mikel Arteta kutokana na kucheza soka la kutumia akili nyingi uwanjani.
Lakini, sasa Havertz ni majeruhi kwa muda mrefu kitu ambacho kimewafanya mashabiki wa Arsenal kumsahau mkali huyo wa Kijerumani.
Straika Jesus naye amerejea uwanjani baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti. Kuna kelele pia za kumtaka Jesus arudi kwa sababu mashabiki wanaamini atakuwa na njaa ya kufanya vizuri. Ni mchezaji anayetumia akili pia anapokuwa ndani ya uwanja na ni fundi. Alifunga kwenye mechi ya kirafiki iliyochezwa bila ya mashabiki alipokabiliana na Watford, hivyo anarudi kumpa changamoto ya namba Gyokeres.
Kisha kuna Merino, ambaye amekuwa akifunga mabao muhimu kwenye kikosi cha Arsenal msimu huu, akifanya hivyo kwenye mechi ngumu.
Chelsea na Newcastle United. Kwenye mechi ambazo kocha Arteta aliwakosa washambuliaji wake wote wa kati ambao ni watatu, basi alimtumia Merino na mtihani mzito kwa mastraika hao akiwamo Gyokeres, kiungo huyo wa Kihispaniola, hakumwaangusha kocha wake. Ameweka mipira kwenye kamba alipotumika kama Namba 9 bandia.
Sasa kurejea kwa Gyokeres kunamfanya Merino kurudi kwenye eneo lake la asili, ambalo ni kiungo huku mashabiki wa Arsenal wakiamini staa huyo wa kimataifa wa Sweden atawafanya kuwa moto uwanjani hata kama kwa sasa hafungi kwa kiwango kinachotarajiwa. Gyokeres anaendelea kubaki kuwa namba moja kwa mashabiki wa Arsenal. Wanampenda na wanaimba nyimbo za kulitaka jina lake.