Arsenal pasua kichwa! Cristhian Mosquera, Declan Rice hoi
Muktasari:
- Wawili hao walipata majeraha wakiwa kwenye jukumu la kuitumikia Arsenal katika mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Brentford iliyopigwa jana Jumatano, Desemba 3, 2025 kwenye Uwanja wa Emirates jijini London, huku wenyeji wakishinda 2-0.
WIMBI la majeruhi limeendelea kuikumba Arsenal, baada ya kocha mkuu wa timu hiyo ya kaskazini mwa jijini London, Mikel Arteta, kuthibitisha kuumia kwa wachezaji Cristhian Mosquera na Declan Rice.
Wawili hao walipata majeraha wakiwa kwenye jukumu la kuitumikia Arsenal katika mechi ya Ligi Kuu ya England dhidi ya Brentford iliyopigwa jana Jumatano, Desemba 3, 2025 kwenye Uwanja wa Emirates jijini London, huku wenyeji wakishinda 2-0.
Mikel Merino na Bukayo Saka waliifungia Arsenal mabao hayo ya ushindi, na kukifanya kikosi cha Arteta kuendelea kuongoza msimamo wa Ligi ya England kwa kufikisha Pointi 33.
Mosquera alilazimika kutolewa uwanjani kipindi cha kwanza akiwa anachechemea na nafasi yake kuchukuliwa na Jurrien Timber, huku Viktor Gyökeres aliingia kuchukua nafasi ya Declan Rice baada ya kupata majeraha.
Arteta amesema ni wakati mgumu sana kwake kuwapoteza wachezaji wengine wawili, hasa katika kipindi hiki muhimu cha kuelekea mwishoni mwa mwaka, wakitanguliwa na William Saliba pamoja na Gabriel Magalhães ambao tayari wameshakosa mechi kadhaa kutokana na majeraha.
“Tumempoteza Saliba, halafu Gabriel, na leo (jana) tumempoteza Mosquera, hili ni pigo kubwa sana kwangu na kwa timu pia, ni vigumu sana kupambana na tatizo hili hasa katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa mwaka ambapo tutacheza michezo kadhaa muhimu.
“Imekuwa changamoto. Ben White ameisaidia sana timu kwenye mechi yetu na Brentford, ameonyesha kiwango cha hali ya juu. Kila mmoja anayepata nafasi ya kucheza anafanya vizuri, nina imani ataendelea kuwa katika hali hii, ili kuziba mapengo ya wachezaji majeruhi.
“Baadae leo tutajua zaidi, kuhusu taarifa za wachezaji Mosquera, Declan baada ya kufanyiwa vipimo, nina imani hawatakuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu sana,” amesema Arteta.
Wachezaji wengine majeruhi katika kikosi cha Arsenal ni Kai Havertz, na Leandro Trossard, hali hii inampa kocha Mikel Arteta changamoto ya kuhakikisha kikosi chake kinaendelea kuwa imara, huku timu ikijitahidi kuendeleza ubora wake kwenye Ligi Kuu ya England.
MECHI ZA ARSENAL MWEZI DESEMBA
Aston Villa vs Arsenal (Desemba 6)
Arsenal vs Wolves (Desemba 13)
Everton vs Arsenal (Desemba 20)
Arsenal vs Brighton (Desemba 27)
Arsenal vs Aston Villa (Desemba 30)