Klopp amfagilia Fabinho

Muktasari:
KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp amemwagia sifa mchezaji wake, Fabinho kwa kusema ni mmoja wa viungo bora kati ya wale ambao wanacheza namba sita baada ya Mbrazil huyo kuisaidia timu hiyo kuichapa RB Leipzig na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa
LONDON, ENGLAND
KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp amemwagia sifa mchezaji wake, Fabinho kwa kusema ni mmoja wa viungo bora kati ya wale ambao wanacheza namba sita baada ya Mbrazil huyo kuisaidia timu hiyo kuichapa RB Leipzig na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, alikuwa muhimili wa Liverpool kwa kutumika kwenye michezo kadhaa kama beki wa kati kufuatia kupata majeraha ya muda mrefu kwa Virgil van Dijk na Joe Gomez lakini kwenye mchezo huo ambao wameibuka na ushindi wamabao 2-0 alichezeshwa kwenye nafasi yake kiasili.
Mabao ya Liverpool kwenye mchezo huo, yalifungwa kipindi cha pili na washambuliaji wao kutoka Afrika, Mohamed Salah na Sadio Mane.
"Kwa kiwango ambacho kilionyeshwa leo kilikuwa cha hali ya juu na kilitakiwa. Tulijilinda vizuri na kwa umakini mkubwa," amesema Kloppa ambaye pia aliongeza kwa kuongelea kiwango cha Fabinho ambaye alijiunga na Liverpool, 2018 akitokea Monaco ya Ufaransa.
"Tutaona kama kutakuwa na ufumbuzi ambao umepatikana lakini namba yake halisi ni namba sita. Ni matumaini yetu kuwa tutaendelea kuwa naye kikosini kwa sababu ni mmoja wa wachezaji bora kwa nafasi ambayo anacheza. Ni mzuri kulinda na hata kushambulia, ni mchezaji muhimu sana kwetu," amesema.
Mbali na Liverpool ambao waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 hivyo kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 4-0, miamba ya soka la Ufaransa, PSG ililazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Barcelona na kutinga hatua hiyo kufuatia ushindi ambao waliupata kwenye mchezo wa kwanza Hispania wa mabao 4-1.
Kwa maana nyingine ni kwamba Barcelona imetupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kipigo cha jumla ya mabao 5-2 dhidi ya PSG.Cristiano Ronaldo akiwa na Juventus yake na Lionel Messi wote wawili timu zao zimeishia katika hatua ya 16 bora.