Kiungo mpya Arsenal aanza kwa masharti
Muktasari:
- Nahodha huyo wa zamani wa Brentford ametua Arsenal katika mazingira ya wengi wakiamini atakwenda kucheza kiungo ya kukabaa kwenye kikosi cha Mikel Arteta kinachotumia 4-3-3.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO mpya wa Arsenal, Christian Norgaard matumani yake ni kuendelea kucheza soka la kushambulia zaidi na siyo kukaba baada ya kukamilisha uhamisho wake wa Pauni 12 milioni huko Emirates.
Nahodha huyo wa zamani wa Brentford ametua Arsenal katika mazingira ya wengi wakiamini atakwenda kucheza kiungo ya kukabaa kwenye kikosi cha Mikel Arteta kinachotumia 4-3-3.
Lakini, mkali huyo wa kimataifa wa Denmark alisema staili yake ya kucheza ni kupanda mbele kwenda kushambuliaji, kwa sababu alianza maisha yake ya soka akiwa mchezaji anayependa kushambulia.
“Nimebadilika tu miaka michache. Nilianza soka nikiwa mchezaji wa kushambulia na sasa nimekuwa nikifanya kazi ya kuwa kiungo wa chini,” alisema Norgaard.
“Kitu muhimu kwangu ni timu kuwa na mfumo mzuri wa kukaba na kwa matumaini makubwa kwa upande wangu, naamini nitachangia hilo. Naamini kocha atanipa uhuru wa kwenda kushambulia.”
Norgaard, 31, amekuwa mchezaji wa tatu mpya kusajiliwa na Arsenal kwenye dirisha hili baada ya kipa Kepa Arrizabalaga na kiungo mwingine Martin Zubimendi, wakifanya matumizi ya timu hiyo kufikia Pauni 77 milioni kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Staa huyo amesaini mkataba wa miaka miwili wenye kipengele cha kuongeza watatu na Arsenal imekubali kuilipa Brentford, Pauni 10 milioni ya awali na Pauni 2 milioni zitalipwa baadaye.
Sasa Arsenal inapambana kukamilisha dili la winga wa Chelsea, Noni Madueke baada ya kufikia makubaliano binafsi na mchezaji huyo, ambaye Jumapili atakuwa na jukumu la kuichezea The Blues kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia la Klabu dhidi ya Paris Saint-Germain.