Kisa Nico, Bilbao yaifanyia vibaya Barca

Muktasari:
- Kwa mujibu wa tovuti ya Cadena Ser, Bilbao imetuma ujumbe kwenda La Liga kushinikiza ukaguzi kamili wa shughuli za kifedha za Barca katika kipindi ambacho timu hiyo inataka kumsajili mchezaji wao.
BARCELONA, HISPANIA: KATIKA harakati za kuhakikisha staa wao Nico Williams anabaki, ripoti zinaeleza Athletic Club inatarajia kuiripoti Barcelona kwa La Liga na kutaka wafanyiwe ukaguzi rasmi wa kifedha kwani inaamini imekiuka sheria.
Kwa mujibu wa tovuti ya Cadena Ser, Bilbao imetuma ujumbe kwenda La Liga kushinikiza ukaguzi kamili wa shughuli za kifedha za Barca katika kipindi ambacho timu hiyo inataka kumsajili mchezaji wao.
Mabosi wa Bilbao wanaamini kwamba timu hiyo haijazingatia sheria ya 1:1 ya ligi, ambayo inaruhusu timu kutumia tu kile ilichozalisha kama mapato.
Williams ameijulisha Bilbao kuwa anataka kuondoka ili ajiunge na Barcelona, lakini Radio Bilbao imeripoti kuwa Athletic iko tayari kupigana kumbakisha, na inasisitiza kuwa haijafikia makubaliano yoyote na winga huyo juu ya kuondoka katika dirisha hili.
Winga huyu ambaye alisaini mkataba mpya Desemba mwaka jana, katika mkataba wake ana kipengele kinachomruhusu kuachiliwa ikiwa timu inayomhitaji italipa Euro 60 milioni.
Rais wa Barca, Joan Laporta aliiambia tovuti ya Mundo Deportivo, kupitia Barca Blaugranes kuwa: “Hatuna uhusiano mbaya na Athletic, ndiyo, kumekuwa na msururu wa kutokuelewana na matukio katika miaka ya hivi karibuni, lakini huwezi kusema tuna uhusiano mbaya, sisi ni timu zenye historia ndefu na uhusiano wa muda mrefu.”
“Naelewa mwelekeo wanaouchukua, kwa heshima yote, kila mtu anapaswa kujihangaikia mwenyewe, lakini sielewi kwa nini wanaenda kuzungumza na La Liga kuhusu Barca, sidhani kama ni sahihi, lakini wao wanajua wanachofanya.”
Alipoulizwa kuhusu sheria ya 1:1, aliongeza: “Tunafanya kazi ili tuendane na sheria ya 1:1.”