Kipigo cha Cameroon chamliza Hugo Broos
Muktasari:
- Kocha wa Bafana Bafana, Hugo Broos, anasisitiza alikuwa na wachezaji sahihi katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, alipokuwa akitafakari kuondolewa kwa kusikitisha katika hatua ya 16-Bora mikononi mwa Cameroon, huku akikiri kikosi hicho kitapitiwa upya kikijiandaa na Fainali za Kombe la Dunia la 2026.
RABAT, MOROCCO: AFRIKA Kusini ilipiga mashuti 18 langoni katika mechi ya 16-Bora juzi usiku dhidi ya Cameroon, lakini ikaweza kufunga bao moja tu, kitu kilichomfanya kocha wa timu hiyo kulia na wachezaji akieleza wamezingua.
Kocha wa Bafana Bafana, Hugo Broos, anasisitiza alikuwa na wachezaji sahihi katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025, alipokuwa akitafakari kuondolewa kwa kusikitisha katika hatua ya 16-Bora mikononi mwa Cameroon, huku akikiri kikosi hicho kitapitiwa upya kikijiandaa na Fainali za Kombe la Dunia la 2026.
Afrika Kusini ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Cameroon juzi mjini Rabat licha ya kutawala sehemu kubwa ya mchezo. Tofauti kubwa ilikuwa ni kwamba Simba Wasioshindika (Indomitable Lions) wa Cameroon walitumia vizuri nafasi walizopata, huku Bafana Bafana wakikosa nyingi.
Umiliki wa mpira wa asilimia 66 wa Afrika Kusini ulizaa mashuti 18 langoni, lakini walichofanikiwa kuonyesha ni bao la kuchelewa la Evidence Makgopa, huku Cameroon ikifunga mabao mawili kutokana na mashuti yao manne yaliyolenga lango.
“Hawa ni wachezaji sahihi kwa wakati huu wa AFCON,” Broos amesema baada ya mechi. “Katika siku na wiki zijazo, itakuwa wakati wa kutathmini AFCON hii, kuona yaliyoenda vizuri na yaliyokwama, na kuhakikisha tunarekebisha mambo mabaya, kwa sababu ndani ya miezi sita kuna Kombe la Dunia.
“Kwa sasa unajisikia mwenye kuchanganyikiwa, huzuni na kukata tamaa na wakati mwingine unasema mambo ambayo baadaye unayajutia. Sitafanya hivyo.”
Broos anaamini timu iliingia uwanjani ikiwa na mpango sahihi wa mchezo, lakini utekelezaji haukuwa mzuri, hasa baada ya mwanzo mzuri ambapo waliipasua safu ya ulinzi ya Cameroon mara kadhaa lakini wakashindwa kulenga lango.
“Nadhani tulikuwa na mpango sahihi. Kipindi cha kwanza tulipata nafasi tatu za wazi kabisa na kwa kawaida mchezo ungetakiwa kuisha hapo,” amesema Broos na kuongeza;
“Lakini unapokosa nafasi hizo, mara nyingi unaadhibiwa. Na sisi tuliadhibiwa kwa bao la bahati. Tuliondoa mpira wa adhabu ndogo nje ya eneo la hatari, mchezaji wao akapiga shuti, kukawa na mipira kugonga miili ya wachezaji, na wakaweza kufunga.
“Kwa bahati mbaya, mapema sana kipindi cha pili wakapata bao la pili, na hapo unajua itakuwa ngumu sana. Tulijaribu kuwa hatari na bado tulipata nafasi. Tulichelewa kidogo kufunga bao letu, na muda haukutosha kusawazisha na kwenda muda wa ziada.
“Kama nilivyosema kabla ya mchezo, Cameroon wanacheza kwa moyo mkubwa, wanapambana na wana uzoefu mzuri na nilijua wangekuwa wapinzani wagumu. Tumeona hilo leo (jana).”
Kwa kufungwa mabao sita katika michezo minne katika mashindano haya, Bafana Bafana walionekana kuwa dhaifu zaidi katika safu ya ulinzi kuliko ilivyokuwa miaka ya karibuni.
Katika AFCON ya 2023 walifungwa mabao matatu tu katika mechi saba na wakamaliza wakiwa na medali ya shaba.
“Ninakubaliana kwamba tumefungwa mabao mengi sana,” Broos amesema. “Tunahitaji kufanya tathmini nzuri ya kilichotokea kwenye mashindano haya na kuangalia mbele kuelekea Kombe la Dunia.”