Hugo Broos kuandika rekodi binafsi Bafana Bafana
Muktasari:
- Rais wa Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA), Danny Jordaan, amempongeza Broos kwa mafanikio hayo, akisema ni hatua kubwa katika taaluma yake ya ukocha.
MARRAKECH, MOROCCO: Kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini maarufu Bafana Bafana, Hugo Broos, anatarajiwa kuweka rekodi binafsi kwa kufikisha mechi 50 akiwa kocha wa timu hiyo, itakayocheza mechi ya kwanza ya fainali za Mataifa Afrika (AFCON 2025) dhidi ya Angola katika Uwanja wa Marrakech, leo Jumatatu, Desemba 22, 2025.
Rais wa Shirikisho la Soka Afrika Kusini (SAFA), Danny Jordaan, amempongeza Broos kwa mafanikio hayo, akisema ni hatua kubwa katika taaluma yake ya ukocha.
“Hongera kwa kocha Hugo kwa kufikia rekodi hii muhimu,” amesema Jordaan.
Broos, anayejulikana kwa mtindo wake wa kusema ukweli bila kuficha, amesifiwa kwa kubadilisha kwa kiwango kikubwa utamaduni wa timu ya taifa kwa zaidi ya miaka minne aliyokaa madarakani, akiichukua Bafana Bafana ikiwa na wachezaji waliokosa kujiamini na timu iliyokuwa imepoteza heshima pamoja na uungwaji mkono wa mashabiki wa Afrika Kusini. Kupitia subira na msimamo thabiti, aliweza kurejesha imani na mshikamano ndani ya kikosi.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa makocha wengi wa timu za taifa, Broos amekumbana na changamoto kadhaa, hasa kuhusu kuwapendelea baadhi ya wachezaji na kukosa uthabiti katika uteuzi wa kikosi.
Miongoni mwa hoja zilizozua mjadala ni kuendelea kumchagua beki Nyiko Mobbie, ambaye baadhi ya wachambuzi wamekuwa wakidai hana mchango mkubwa kwenye timu, pamoja na uamuzi wa hivi karibuni wa kumuacha nje Thembinkosi Lorch kwenye kikosi cha AFCON 2025.
Hata hivyo, Broos ameendelea kusimamia msimamo wake, licha ya kupata changamoto ya kukosolewa na wachambuzi, ambao amekuwa akiwashangaza kwa matokeo ya uwanjani.
Broos aliikuta Bafana Bafana ikiwa nafasi ya 75 katika viwango vya ubora vya FIFA, lakini kwa sasa ameipandisha hadi nafasi ya 61, huku ndoto ya kuingia ndani ya timu 50 bora duniani ikionekana kuwa karibu zaidi kutimia.
Chini ya uongozi wake, Afrika Kusini imepata medali ya shaba katika fainali za AFCON 2023 zilziofanyika nchini Ivory Coast. Broos anatarajiwa kustaafu baada ya Kombe la Dunia la FIFA 2026, litakalofanyika Marekani, Mexico na Canada.
Mei 5, 2025, Broos aliweka historia kwa kufikisha miaka minne kamili akiwa kocha wa Bafana Bafana, hivyo kuvunja au kulingana na rekodi ya marehemu Clive Barker, aliyekuwa kocha wa muda mrefu zaidi wa timu hiyo.
Barker aliiongoza timu hiyo kuanzia Januari Mosi, 1994 hadi Januari Mosi, 1998 na aliipa Afrika Kusini ubingwa wao wa kwanza wa AFCON mwaka 1996. Kwa sasa Broos ndiye kocha aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya timu hiyo.
Kwa sasa, Bafana Bafana inachukuliwa kama timu inayopaswa kuogopwa barani Afrika, kufuatia rekodi ya kocha huyo raia wa Ubelgiji ya kupata ushindi mara 24, sare 19 na vipigo sita pekee.