Kina Haaland warudisha pesa za mashabiki
Muktasari:
- Kwa kuwa tiketi ya ugenini kwa mchezo huo ilikuwa ikigharimu takribani Pauni 25, wachezaji wa Man City watachangia jumla ya Pauni 9,357 ili kuwalipia mashabiki wote waliokwenda hadi Kaskazini ya Aktiki (Arctic Circle).
MANCHESTER, ENGLAND: MASTAAA wa Manchester City wamekubaliana watalipa gharama za tiketi kwa mashabiki 374 waliosafiri hadi Norway kushuhudia kipigo cha kushangaza cha mabao 3-1 kutoka kwa Bodoe/Glimt kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Jumanne iliyopita.
Kwa kuwa tiketi ya ugenini kwa mchezo huo ilikuwa ikigharimu takribani Pauni 25, wachezaji wa Man City watachangia jumla ya Pauni 9,357 ili kuwalipia mashabiki wote waliokwenda hadi Kaskazini ya Aktiki (Arctic Circle).
Wakizungumza kwa niaba ya kikosi, kundi la manahodha wa Man City, Bernardo Silva, Ruben Dias, Rodri na Erling Haaland wamesema: “Mashabiki wetu ni kila kitu kwetu. Tunafahamu kujitolea kunakofanywa na mashabiki wetu wanaposafiri kote duniani kutuunga mkono nyumbani na ugenini na hatutachukulia hilo kama jambo la kawaida kamwe. Wao ni mashabiki bora zaidi duniani.
"Pia tunatambua ilikuwa safari ndefu sana kwa mashabiki waliotuunga mkono kwenye baridi kali wakati wa usiku mgumu kwetu uwanjani. Kulipia gharama za tiketi kwa mashabiki waliosafiri hadi Bodoe ni jambo dogo zaidi tunaloweza kufanya.”
Hatua hiyo imesifiwa na Chama Rasmi cha Mashabiki (OSC) cha klabu, licha ya kuwepo kwa wito mdogo tu kutoka kwa mashabiki uliotaka kurejeshewa fedha.
Mwakilishi wa OSC ya Manchester City, Kevin Parker, amesema: “Mashabiki wa Man City wanasafiri hadi mwisho wa dunia kuiunga mkono timu yetu na usiku uliopita haikuwa tofauti, hata ndani ya Mduara wa Aktiki. Bodoe si mahali rahisi kufika na joto lililokuwa chini ya sifuri lilifanya usiku huo kuwa mgumu kwa mashabiki wetu kwa viwango vingi. Uhusiano kati ya wachezaji na mashabiki wa Man City siku ya mechi ni wa kipekee sana na hatua hii ni ukumbusho mwingine wa uhusiano huo inamaanisha mengi sana kwetu.
"Tunajua wachezaji wamesikitishwa na kipigo dhidi ya Bodoe, lakini kwa mchezo wetu ujao nyumbani Jumamosi, kuna nafasi ya kurejea kwenye ushindi na mashabiki wetu watakuwa na sauti kubwa.”
Man City ilikumbana na moja ya mshtuko mkubwa zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kushindwa na Bodoe/Glimt, na sasa inahitaji ushindi katika mchezo wao wa mwisho wa awamu ya ligi dhidi ya Galatasaray ili kuhakikisha wanamaliza ndani ya nane bora.